Wasiliana Nasi

Wasiliana Nasi

Tuesday, March 3, 2015

TUUNGANE KUTOKOMEZA UKATILI WANAOFANYIWA NDUGU ZETU ALBINO


Elnest Mangu.

Hakika Mungu ni wa ajabu kwa sababu anatupenda wote bila ubaguzi, hivyo hatunabudi kumhimidi milele. Baada ya kusema hayo niseme wazi kwamba leo napenda nizungumzie suala la kuhuzunisha la mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, wengine huwaita Maalbino.

Hili suala linasikitisha sana licha ya ukweli kwamba limekuwa likipigiwa kelele kila kukicha lakini hatua zinazochukuliwa hazina uzito ukilinganisha na tatizo lenyewe.Watu wanaofanya vitendo vya kuwaua au kuwakata viungo vyao hakika si binadamu wa kawaida, wana roho ya kinyama. Fikiria kama mtu anamkuta Albino anamkata kiungo cha mwili wake kwa kudanganywa kuwa eti ni mali! Ujinga gani huu ndugu zangu?

Tena kwa wengine haitoshi wanaamua kuondoa uhai wao kabisa, yaani wanaua Albino, kusema kweli inauma, inasikitisha na kuhuzunisha.Jambo la kusikitisha ni kwamba vyombo vya dola havijaweka mkakati wa kutokomeza mauaji haya kwani kila yanapotokea utasikia matamko ya viongozi wakisema ‘tunafanya uchunguzi kubaini watu waliofanya hivyo.’

Ipo haja ya kuweka mikakati ya kuhakikisha tatizo hili linakwisha kwa sababu inawezekana wanaofanya vitendo hivi vya kuua au kukata viungo Albino wapo miongoni mwa jamii yetu.Kusema ‘tunafanya uchunguzi’, hakutoshi kwa sabau kauli hiyo inaonekana kama ya kuwatuliza tu waathirika. Baada ya muda kukitulia kila mtu anaendelea na shughuli zake.

Baada ya siku kadhaa tunasikia tena tukio la kukatwa Albino kiungo au kunyakuliwa mgongoni mama mwenye mtoto mwenye ulemavu huo wa ngozi. Hali inatisha. Tujiulize mwisho wa haya mambo ni lini?
Wale wanaoguswa hasa majirani utasikia wakitoa kauli za kukemea mambo hayo. Wengine hufikia hatua ya kuwalaumu wenyeji kutokana na jinsi wanavyochukulia kiurahisi suala hilo.

Niipongeze nchi ya Uturuki iliyoamua kujenga kituo cha watoto wenye ulemavu wa ngozi. Hatua hiyo ilikuja baada ya kushamiri kwa matukio ya aina hiyo. Huenda kituo hicho kitakamilika mwaka huu ambapo watoto zaidi ya 500 wenye ulemavu wa ngozi watakuwa wakiishi kituoni hapo na kupewa huduma zote.

Inawezekana wenyeji wamefanya jitihada fulani kutokomeza hilo lakini bado nguvu zaidi inahitajika kwa upande wa serikali na jamii kwa ujumla.Waturuki wameonyesha upendo kwa Tanzania na kwa jamii hiyo yenye ulemavu wa ngozi lakini tusifurahie kwa sababu inawezekana wamefanya hivyo kwa kutubeza na kutuona wajinga kumbe wajinga ni wachache, wale wanaoagiza au kutekeleza maagizo ya kutafuta kiungo cha Albino kwa sababu za kishirikina.

Niwaeleze wale wenye ujinga wa kufikiri kwamba Albino ni binadamu kama wengine hivyo wote tuungane kuwasaka wanaojihusisha na unyama huu na kamwe tusisuse au kuchangia kwa namna yoyote kulipa kisogo tatizo hili.

Takwimu za kutoka mwaka 2006 zinaonyesha kuwa Albino 76 wameshauawa kikatili, huku 56 wakinusurika kifo na kati yao 11 wameongezewa ulemavu mwingine wa kudumu kwa kukatwa viungo vyao. Vilevile makaburi 18 ya watu wenye ulemavu wa ngozi yamewahi kufukuliwa kwa imani za kishirikina kwamba viungo vyao vinawapa utajiri baadhi ya watu na uongozi. Jamani ujinga huu utaendelea mpaka lini?

Licha ya matukio yote hayo yakinyama bado utasikia vyombo vya usalama vikisema ‘tutachukua hatua’, je hatua hizo ni zipi? Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Ernest Mangu weka mikakati, tushirikishe raia wote, tutafanikiwa. Nchi jirani zimetupachika majina ya kila aina kutoka na vitendo hivyo vya kikatili vinavyofanywa na Watanzania wenzetu wenye roho mbaya. Heshima, ukarimu na upendo tulionao unaonekana kama ni wa kinafiki katika nchi hizo. Mnataka jamii ya Albino waishi kwenye nchi yao kama wakimbizi?
Wote tuseme, inatosha. Tuungane kutokomeza mauaji ya Albino.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

0 comments:

Post a Comment