Wasiliana Nasi

Wasiliana Nasi

Wednesday, March 25, 2015

KIFUA KIKUU: UGONJWA UNAOUA ZAIDI YA WATU MILIONI 1 DUNIANI KILA MWAKA


Mgonjwa wa kifua kikuu akipatiwa matibabu.


KWA Tanzania, watu 120,191 hukisiwa kuwa na ugonjwa wa kifua kikuu kila mwaka, hii ni kutokana na taarifa ya Shirika la USAID ya mwaka 2007 na vifo vinavyotokana na ugonjwa wa kifua kikuu ni 32,000 kila mwaka hapa nchini Tanzania.


Muonekano wa mapafu ya binadamu yaliyoathirika kwa TB.


Takwimu za Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) zinaonyesha kuwa Tanzania ni ya 15 kati ya nchi 22 ambazo zimeathiriwa sana na ugonjwa huu na kwa mujibu wa takwimu za shirika hilo, kwa dunia nzima mwaka 2012 watu milioni 8.6 waliambukizwa ugonjwa wa kifua kikuu, na watu milioni 1.3 walifariki kwa ugonjwa huo wengi kutoka katika nchi
zinazoendelea.

Ugonjwa huu huathiri asilimia 98 ya watu katika nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania.

SIKU YA KIFUA KIKUU DUNIANI

Kwa nyakati tofauti, walimwengu wakiwamo wanasayansi walikaa na kukubaliana hivyo kuanzisha Siku ya Kifua Kikuu duniani, Machi 24.
Siku hiyo ni mahsusi kwa ajili ya kufanya mapitio kuhusu hali halisi ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo.



KIFUA KIKUU NI NINI

Kitaalamu, unaelezwa kuwa ni ugonjwa wa kuambukiza kutoka mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwa njia ya hewa.
Inaelezwa kuwa mtu menye vijidudu vya ugonjwa huo akihoa, kupiga chafya au kwa namna yoyote nyingine kurusha vitone vya makohozi yake kutoka katika mfumo wake wa hewa na kuvieneza hewani na mtu mwingine kumpata akivuta hewa ndani na hivyo kuingia katika mfumo wa hewa.

Ugonjwa wa kifua kikuu ni kati ya magonjwa matatu yanayotokea kwa kiasi kikubwa na kuwapata watu masikini zaidi.

CHANZO AU SABABU ZA KIFUA KIKUU

Ugonjwa huu husababishwa na bakteria waitwao, Mycobacteria tuberculosis.
Kuna aina nyingi za jamii hii ya Mycobacterium kama Mycobacteria tuberculosis (ambao husababisha kifua kikuu), Mycobacteria leprae (wao husababisha ugonjwa wa ukoma), Mycobacteria bovis (huathiri ng’ombe na binadamu), Mycobacteria afrikanum na wengineo.


Mycobacteria tuberculosis (ambao husababisha kifua kikuu).

Ugonjwa wa Kifua Kikuu unaweza kuathiri mapafu, mishipa ya fahamu, mifupa, mfumo wa mzunguko wa damu, ngozi, viunganishi vya mifupa (joints) na mfumo wa tumba zakuchuja vimelea vya maradhi(lymphatic system.

Mycobacteria bovis ambao huathiri ng’ombe, ni jami inayoweza kuambukiza pia binadamu kama atakula nyama au bidhaa zinazotokana na maziwa ya ng’ombe ambayo yameathirika na bakteria hawa.

Mazao mengine ya mifugo kama vile siagi, mtindi, maziwa yenyewe, cheese, ice cream na kadhalika, yanaweza kumdhuru mwanadamu endapo yalikuwa na virusi hao.

Aina hii ya bakteria huathiri mapafu, tezi (lymph nodes), tumbo na sehemu nyingine za mwili.
Wataalam wanaeleza kuwa asilimia 10 tu ya watu walio na bakteria hao jamii ya Mycobacteria tuberculosis hawapati ugonjwa huu wa Kifua Kikuu.

AINA ZA KIFUA KIKUU

Kuna aina kuu tatu za ugonjwa wa Kifua Kikuu;

-Kifua kikuu kinachosababisha madhara (active tuberculosis) – Huu hutokea pale ambapo bakteria waliopo mwilini wapo hai na kinga ya mwili imeshindwa kuwadhibiti hawa

bakteria wasisababishe madhara. Watu hawa wanaweza kumuambukiza mtu yoyote kifua kikuu kwa njia ya kuvuta pumzi kama watakohoa, kutema mate, kupiga chafya, kupiga kelele iwapo watafanya vitendo hivi karibu na watu wasio na ugonjwa huu.

-Ugonjwa usiosababisha madhara (inactive tuberculosis) – Kwa kitaalamu huu pia huitwa Latent TB. Hapa inaamaanisha kuwa kinga ya mwili imeweza kuwadhibiti bakteria na kuwafanya kushindwa kusababisha madhara.
Mtu mwenye Latent TB, hana dalili za ugonjwa huu, hajisikii mgonjwa na hawezi kuambukiza mtu mwingine ugonjwa wa kifua kikuu.

Aina hii inaweza kujirudia baadaye na kuathri sehemu ya juu ya mapafu na hivyo kusababisha kikohozi cha kawaida ambacho baadaye huongezeka na kusababisha kikohozi cha damu au makohozi, homa, kupungua hamu ya kula, kupungua uzito bila sababu ya msingi na kutokwa jasho kwa wingi kuliko kawaida wakati wa usiku.

-Ugonjwa uliosambaa mwilini (milliary tuberculosis) – Hii hutokea pale ambapo kinga ya mwili imepungua na kusababisha ugonjwa wa kifua kikuu kuenea kupitia damu hadi sehemu nyingine za mwili kama mifupa, mishipa ya fahamu, ngozi, figo, kibofu cha mkojo, ngozi ya moyo (pericadium), mfumo wa uzazi, viunganishi vya mifupa (joints) na lymphatic system. Husababisha homa, kupungua hamu ya kula, kuchoka na kupungua uzito.

VIHATARISHI VYA UGONJWA HUU NI;

-Uzee
-Unywaji pombe kupindukia
-Kuishi sehemu zilizo na mrundikano wa watu kama mabweni, kambi za jeshi, hospitali, mabasi ya abiria.
-Magonjwa yanayoathiri kinga ya mwili kama Kisukari.
-Wafanyakazi wa huduma ya afya
-Ugonjwa wa Ukimwi
-Utapiamlo
-Umaskini au hali duni ya kipato
-Kuishi kwenye nyumba za jamii, mfano nyumba za wazee
-Wale wasio na makazi
-Baadhi ya dawa – Dawa za ugonjwa wa maumivu ya mifupa (athritis)
-Wasafiri au watalii kutoka nchi zilizo na idadi kubwa ya ugonjwa wa kifua kikuu.



DALILI NA VIASHIRIA VYA UGONJWA WA KIFUA KIKUU
-Kukohoa zaidi ya wiki 2-3 na kuongezeka kutoa makohozi
-Kukohoa damu
-Homa za mara kwa mara
-Kupungua au kukosa hamu ya kula
-Kupungua uzito kwa asilimia 10.
-Kutokwa na jasho kwa wingi hasa wakati wa usiku
-Uchovu
-Maumivu makali ya kichwa
-Maumivu ya kifua
-Kupumua kwa shida



VIPIMO VYA KIFUA KIKUU NA MATIBABU
-Kipimo cha makohozi (Sputum for AFB) – Makohozi huchukuliwa kwa siku tatu mfululizo muda wa asubuhi na kupelekwa maabara kufanyiwa uchunguzi ili kuweza kugundua kama mtu ana TB.
-Kwa wale wagonjwa wasioweza kutoa makohozi au wale wenye TB ya tumbo, basi hufanyiwa kipimo cha gastric lavage.
-Matibabu ya kifua kikuu ni bure katika hospitali zote za serikali na binafsi. Unapoona mtu ana dalili mojawapo za kifua kikuu au wewe mwenyewe mshauri awahi kituo cha huduma za afya kwa uchunguzi na tiba kwani mtu mmoja huweza kuwaambukiza watu kati ya 10 hadi 15 kwa mwaka kama hajapata matibabu.
-Ikitokea umegundulika kuwa una kifua kikuu usihofu kwani kinatibika na mamilioni ya watu duniani kote wameugua na kupona. Unachotakiwa kufanya ni kufuatisha masharti utakayopewa na daktari kama; kunywa dawa kila siku kwa muda uliopangiwa ili kupona kabisa.
-Matibabu yake huchukua kati ya miezi sita hadi minane.

JINSI YA KUKABILIANA NA KIFUA KIKUU
-Jambo la msingi na muhimu ni kuwahi kufika katika huduma za afya mapema mara unapohisi dalili za kifua kikuu.
-Zingatia matibabu pale unapoanza kutumia dawa za kifua kikuu na hakikisha unatumia dawa kama ulivyoelekezwa na wataalamu wa afya, kumbuka usugu wa dawa na kushindwa kwa dawa hizi ni hatari zaidi katika kupambana na ugonjwa huu.
-Usiache kutumia dawa za kifua kikuu ili kuepuka kupata TB sugu na ile isiyotibika kwa dawa mchanganyiko.
-Hakikisha pale unapoona unakohoa zaidi ya wiki mbili unafika katika huduma za afya kwa ajili ya uchunguzi na matibabu.
-Funika mdomo na pua kwa kitambaa pale unapokohoa au kupiga chafya hii inasaidia kuzuia kuenea maambukizi.
-Kuepuka mikusanyiko au mrundikano wa watu kama vile kwenye mabweni, kambi za jeshi, baa na kadhalika.
-Kuishi kwenye nyumba ambayo ina mfumo mzuri wa kuingiza na kutoa hewa yaani iwe na madirisha makubwa na ya kutosha.
-Pia, kuishi katika mienendo bora inayozingatia afya, kula mlo kamili, kunywa maji mengi angalau lita 1.5 kwa siku na mazoezi mepesi kama kutembea kwa dakika 15 kwa siku yanachangia kuujenga mwili na kuwa wenye afya njema.
-Pata mapumziko ya kutosha angalau lala masaa sita kwa siku, epuka matumizi ya ulevi wa pombe.

0 comments:

Post a Comment