Wasiliana Nasi

Wasiliana Nasi

Tuesday, March 17, 2015

MTOTO ALIYENUSURIKA KWA MKONO WA MUNGU! AJALI YA KONTENA MAFINGA

Na Mwandishi Wetu, Iringa
BADO Mji wa Mafinga wilayani Mufindi mkoani hapa haujakaa sawa kufuatia vifo vya watu 50 waliopoteza maisha kwa ajali ya kontena kudondokea Basi la Majinja lenye namba za usajili T 438 CED iliyotokea Machi 11, 2015, Uwazi limechimba.

Mtoto aliyenusurika kwenye ajali.

Ajali hiyo ilitokea maeneo ya Changarawe mjini Mafinga ambapo kontena hilo lilikuwa kwenye lori la mizigo la Scania lenye namba za usajili T 689 APJ mali ya Kampuni ya Cipex lililokuwa likitokea Dar kwenda Mbeya huku basi hilo likitokea Mbeya kuelekea Dar.

KILICHOTOKEA BAADA YA AJALI
Kilichotokea baada ya ajali hiyo ni kuonekana kwa Mkono wa Mungu ambapo mtoto anayekadiriwa kuwa na umri wa mwaka mmoja mpaka miwili kunusurika katika ajali hiyo huku watu 50 wakipoteza maisha.
“Mimi naweza kusema ni Mkono wa Mungu kwa sababu, yule mtoto alikutwa hajaumia popote lakini wazazi wake wakiwa wamepoteza maisha. Huoni kama ni uwezo wa Mungu mwenyewe?” alisema askari polisi mmoja aliyekuwa miongoni mwa waliokuwa wakisimamia zoezi la uokoaji.

WAZAZI WA MTOTO
Akisimulia ilivyokuwa kwa wazazi wa mtoto huyo ambaye jina lake halijajulikana, mmoja wa abiria walionusurika, Aidan alisema kuwa, kabla ya kuanza safari jijini Mbeya, mtoto huyo alibebwa na mama yake akiwa ameongozana na abiria wengine.

Muonekano wa kontena lililosababisha ajali hiyo.

“Wazazi wa mtoto waliingia na kukaa siti ya tatu tu kutoka kwa dereva. Hakuna aliyehisi kwamba mbele ya safari kuna janga kubwa kama hili.“Basi lilianza safari, kila abiria alikuwa akizungumza na mwenzake, wengine walikuwa wakiongea na simu. Wapo waliokuwa wakichati, nadhani ni wale wanaotumia WhatsApp. Kumbe bwana shetani alikuwa anatembea na sisi,” alisema abiria huyo akiwa kwenye Hospitali ya Wilaya ya Mufindi.

KABLA YA AJALI
Kwa mujibu wa majeruhi mwingine wa ajali hiyo, baada ya kufika eneo la Changarawe, kwa mbele lilionekana lori hilo likiwa katika mwendo wa kawaida na hakuna aliyewaza kwamba litaangukia basi lao.

“Mbele tuliliona lile lori likija, lakini mimi nimekuwa nikisafiri mara kwa mara kwa kutumia barabara hiyo. Najua eneo hilo lina shimo lakini sikuwa na wazo kwamba shimo lile litakuwa mtoa roho wa abiria wa basi letu.
“Wakati tunapishana sasa, lori linapita kulia kwetu, mimi nilikaa siti ya nyuma upande wa abiria. Ghafla nilishtuka kuona kama giza linatanda upande wa dereva, mara nikasikia watu wakianza kulia.

“Kabla sijajua ni nini, nikasikia kishindo kikuu. Puuu! Abiria wengine walisikika wakisema wanakufa, wengine wakiwa kimya! Ndipo nikajua tumeangukiwa na kontena lakini sikuweza kufuatilia ilikuaje kwani akili zikawa kama zimeniruka,” alisema abiria huyo bila kutaja jina lake.


Mabaki ya basi la Majinja baada ya ajali.

KILICHOMTOKEA MTOTO HUYO
Baadhi ya waokoaji waliofika mapema mara baada ya ajali hiyo waliliambia Uwazi kwamba, wakati wanahangaika kuitoa miili ya majeruhi na marehemu, walishangaa kumkuta mtoto huyo akiwa chini ya siti ya nyuma kabisa maarufu kwa jina la ‘kwa balozi’, akiwa hana michubuko.

“Baadhi ya abiria walionusurika wakatuambia huyu mtoto alikaa na wazazi wake kwenye siti ya tatu kutoka kwa dereva. Sasa amefikaje kule nyuma kwa balozi? Nadhani anayejua ni Mungu.“Unajua watoto wadogo wana mkono unaowalinda. Mara nyingi katika ajali wao wanasalimika kwa njia ya ajabu sana,” alisema askari mmoja wakati wa uokoaji.

Picha ya mtoto huyo ilipigwa na mpiga picha Francis Godwin kwenye Wadi Namba 3 kwa kusaidiwa maelekezo na polisi wa kike na muuguzi mmoja aliyekuwa na orodha ya watu walionusurika. Watu wengine wawili kitandani hapo walikuwa ni wasamaria wema waliokuwa wakimsaidia mtoto huyo ambapo wazazi wake wanasadikiwa walipoteza maisha.

Polisi wakiwa eneo la tukio.

MGANGA MKUU NA MKUU WA MKOA
Juzi, Uwazi lilizungumza na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Salimin Mahimbo kuhusu ajali hiyo ambapo alisema mpaka sasa, majeruhi waliolazwa ni saba baada ya mmoja kufariki dunia na majeruhi mwingine kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kutokana na hali yake kuzidi kuwa mbaya.

“Mpaka sasa tuna majeruhi saba tu, mmoja alifariki dunia. Mmoja amekimbizwa Muhimbili kwa matibabu zaidi, hali yake si nzuri, hawa saba wanaendelea vizuri,” alisema Mahimbo.Naye Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alisema mpaka juzi, marehemu wote walishatambuliwa na ndugu zao na waliolazwa wametambuliwa pia.

0 comments:

Post a Comment