Wasiliana Nasi

Wasiliana Nasi

Thursday, March 12, 2015

KADA WA CHADEMA AUAWA KWA KUPIGWA MSHALE WA TUMBONI


Mwili wa kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Marwa Omtima ukizikwa.

IGENGA MTATIRO, TARIME

MKAZI wa Kitongoji cha Nyaiheta, Kijiji cha Kewanja Kata ya Kemambo wilayani Tarime, Mara, Marwa Omtima (55) ambaye ni kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ameuawa kwa kupigwa mshale tumboni na mtu aliyetajwa kwa jina la Gamaina, mkazi wa kitongoji hicho kulipotokea ugomvi usiku wa Machi 5, mwaka huu.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Tarime na Rorya limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema siku ya tukio, marehemu alipigwa mshale majira ya usiku na kufariki dunia.


Mwili wa Marwa ukiagwa.

Jeshi hilo lilisema linaendelea kumsaka mtu aliyefanya mauaji hayo ili kumkamata na kumfikisha mahakamani kujibu tuhuma zake za kuua huku chanzo kilidaiwa ni ugomvi binafsi uliotokana na chuki za siku zilizopita.

Ilielezwa kuwa, marehemu alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Wilaya ya Tarime baada ya kuvuja damu nyingi.Katika mazishi yaliyofanyika Machi 7, mwaka huu, msemaji wa familia hiyo ambaye ni kaka wa marehemu Omtima, Masanda Omtima, aliwaambia waombolezaji kuwa, familia haitakuwa na kisasi na familia ya mtuhumiwa.

Aliwaomba wanafamilia wa pande zote kuendelea kutembeleana kama zamani huku akisema ni dhambi kuua mtu kwani aliye na mamlaka ya kuondoa uhai wa binadamu ni Mungu.Kutokana na tukio hilo, Mkuu wa Kituo cha Polisi Nyamwaga aliyehudhuria mazishi hayo, OCD Simon Marwa Maigwa alisema atahakikisha muuaji huyo anasakwa mahali popote alipokimbilia na kutiwa nguvuni.

Miongoni mwa waombelezaji wa msiba huo walioshindwa kutoa ujumbe wao kwa simanzi ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Esther Nicholas Matiko aliyesema tukio hilo limetia aibu na kuichafua Mara.



Matiko alisema imefikia wakati jamii kubadilika kwa kutumia njia za kisheria badala ya kujichukulia sheria mikononi na kusababisha marehemu kuacha familia iliyomtegemea ikitaabika.Kwa upande wake, Katibu wa Chadema Mkoa wa Mara, Chacha Heche aliwaomba viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na wale wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutumia muda wao kuelimisha jamii kuacha kuchukua sheria mikononi.

Mazishi hayo yaliyovuta hisia za watu wengi kutoka vyama vya siasa na viongozi wake, jamii na askari polisi kwani aliyeuawa kaka yake ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Kewanja Tanzania, Omtima (Chadema).

0 comments:

Post a Comment