Wasiliana Nasi

Wasiliana Nasi

Friday, April 17, 2015

UVIMBE WA KIZAZI (UTERINE FIBROID)




Fibroid ni uvimbe unaoota ndani ya kizazi cha mwanamke, uvimbe huu upo kama nyama laini, chanzo halisi cha aina hii ya uvimbe bado hakijulikani lakini ni tatizo linalosumbua zaidi wanawake walio katika umri wa kuzaa.
Umri wa kuzaa ni ule kuanzia pale mwanamke anapovunja ungo hadi anapofikia ukomo wa kuzaa.

Umri wa kuvunja ungo ni kati ya miaka kumi na mbili hadi kumi na tano, hapa tunategemea mwanamke anaweza kuvunja ungo lakini anaweza kuwahi au kuchelewa.Umri wa mwisho kuzaa ni kuanzia miaka arobaini na tano na kuendelea hadi hamsini. Mwanamke kuendelea kutokwa na damu ukeni zaidi ya umri wa miaka hamsini wakati mwingine inakuwa si hali ya kawaida.

Chanzo cha tatizo
Kama tulivyoelezea hapo juu, chanzo halisi hakijulikani, yaani huwa inatokea tu kutokana na mabadiliko ya mwili wa mwanamke, mabadiliko haya yanahusisha mfumo wa homoni wa mwanamke pamoja na chembe hai za kizazi.

Tatizo pia huwapata zaidi wanawake weusi kuliko wazungu, yaani maeneo ya Afrika, India na Amerika. Vilevile tatizo huwatokea zaidi wanawake ambao hawajashika ujauzito au hawajawahi kuzaa kabisa hadi wanapofikia umri wa kati, kuanzia miaka 28 na kuendelea.

Wanawake ambao wameshazaa hupatwa na tatizo hili lakini mara chache kulinganisha na wale ambao hawajazaa kabisa au walishazaa mtoto mmoja au wawili na wakakaa muda mrefu bila ya kuzaa, nao hukabiliwa na tatizo hili.

Aina za uvimbe wa fibroid
Uvimbe wa Fibroid au Uterine Leiomyoma au Uterine Myoma umegawanyika katika sehemu kuu tatu. Unaotokea ndani ya kizazi, unaotokea katikati ya misuli ya kizazi na unaotokea nje ya kizazi.
Uvimbe huu pia unaweza kuchomoza katika mdomo wa kizazi au ukaning’inia ndani au nje ya kizazi.

Dalili za tatizo
Uvimbe wa Fibroid huanza taratibu bila mwanamke kujua, unapoendelea kukua utahisi kuna kitu kizito na kigumu chini ya tumbo, baada ya muda utahisi maumivu. Uvimbe huu huambatana na kupata damu nzito ya hedhi na maumivu. Damu hii hutoka kidogokidogo kwa muda mrefu kuliko ulivyozea mzunguko wako .
Hali inaweza kuendelea hivyo na ukajikuta unaishiwa damu na mwili unakuwa dhaifu.

Maumivu ya tumbo na uzito chini ya tumbo vikiendelea unajikuta unapata haja ndogo mara kwa mara, unafunga kupata choo kikubwa na mwishowe tumbo linakua kubwa kama mjamzito.Mzunguko wa hedhi unavurugika kiasi kwamba hujui siku zako ni lini na uwezo wa kushika mimba unapotea.

Athari za uvimbe
Uvimbe huu huwa unakua mkubwa na kukusababishia maumivu. Uvimbe ukiwa ndani ya kizazi unaweza usipate mimba kabisa. Uvimbe ukiwa katika misuli ya kizazi unaweza kupata mimba na isiendelee baadaye ikatoka, uvimbe ukiwa nje ya kizazi athari zake ni kupata maumivu makali sana wakati wa ujauzito na ukajikuta mimba inatoka au itakubidi uzae kwa upasuaji.

Athari kubwa nyingine ya uvimbe upasuaji wake ni wa kuondoa kizazi kwa kuwa kunakuwa hakuna jinsi. Kwa hiyo unajikuta huna mtoto na umechelewa kutibiwa na uvimbe umekua mkubwa hivyo huna budi kuondolewa kizazi.Uvimbe wa Fibroid usipodhibitiwa unakua mkubwa sana kwa haraka, ukuaji wake unategemea kiwango kikubwa cha homoni ya Estrogen mwilini.

Uchunguzi
Mara nyingi mwanamke anagundulika na tatizo la fibroid kama ataenda hospitali kwa lengo la kutafuta ujauzito, maumivu ya tumbo chini ya kitovu kwa muda mrefu, maumivu wakati wa tendo la ndoa, kuvurugika kwa mzunguko wa hedhi hivyo, vipimo mbalimbali vitafanyika Baada ya uchunguzi wa kina ndipo matibabu hupangwa.

Matibabu na ushauri
Tiba hufanyika baada ya uchunguzi wa kina kuona kama uvimbe upo vipi na una ukubwa gani. Uvimbe mdogo unaweza kutibika kwa dawa huku mwanamke akipewa msisitizo abebe ujauzito, uvimbe mkubwa lazima upasuaji ufanyike. Wahi hospitali kwa uchunguzi na tiba.

0 comments:

Post a Comment