Wasiliana Nasi

Wasiliana Nasi

Thursday, April 2, 2015

SOKO LA BUGURUNI: SHILINGI MIL.27 HUKUSANYWA KWA MWEZI, LAKINI HALI YA UCHAFU SOKONI HAPO NI HATARI

Na Makongoro Oging’
Soko la Buguruni ni moja kati ya masoko makubwa yanayotegemewa katika Jiji la Dar es Salaam kwa serikali kujipatia kipato pia wateja kujipatia mahitaji ya kila siku lakini cha kushangaza ni kwamba uchafu umekithiri.

Muonekano wa soko la Buguruni.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa soko hilo, Said Habibu Kondo amesema soko hilo lina wafanyabiashara 3,000 na kila mmoja hutozwa ushuru na manispaa kati ya shilingi 300 hadi 400 kwa siku ambapo kwa mwezi zinakusanywa zaidi ya shilingi milioni 27,000,000.

Hata hivyo, fedha hizo hazisaidii katika ukarabati au uzoaji wa taka sokoni hapo.
Uchunguzi uliofanywa na Fukunyuafukunyua sokoni hapo umegundua kwamba wafanyabiashara na wateja wao wako hatarini kiafya ikiwa ni pamoja na hatari ya kulipuka kwa ugonjwa wa Kipindupindu kutokana na uchafu uliokithiri kila kona huku manispaa ikilegalega katika uzoaji wa taka.

BIDHAA JUU YA YA MATOPE
Wafanyabiashara hao walionekana wakipanga bidhaa juu ya matope na uchafu ukiwa umefunikwa na inzi wa kila aina hali inayowafanya baadhi ya wateja kususa kununua na kuamua kurudi nyumbani bila kitu.

“Manispaa ya Ilala imekuwa mstari wa mbele katika ukusanyaji wa ushuru kila siku bila kukosa lakini kwa uzoaji wa taka wamekuwa wakitokea mara moja moja jambo ambalo ni hatari kwa afya zetu na walaji pia,” alisema mfanyabiashara aliyejitambulisha kwa jina la Chuku Hamisi.

“Angalia tunavyonyeshewa mvua, matunda mengi yameoza, manispaa haitaki tuweke maturubai wala mabati mapya,wameshindwa kutulinda kiafya, fedha zinazokusanywa hatujui zinafanya kazi gani nina wasiwasi huenda zinaliwa,” alisema Chuku.

Uchafu uliokithili kwenye soko hilo.

Wafanyabiashara hao waliendelea kusema kwamba manispaa hawana haya, wanakusanya ushuru katika uchafu,walidai kwamba kati ya fedha zinazokusanywa hapo walitakiwa kutoa asilimia kumi kwa ajili ya soko hilo lakini inasemekana hata siku moja hawajafanya hivyo.

“Zamani kulikuwa na mkandarasi aliyekuwa akifanya kazi ya usafi na ukusanyaji wa taka ambapo hali ya soko ilikuwa nzuri lakini tangu waingie mgogoro na manispaa hali ni mbaya sana kwani kumekuwa na rundo la takataka kwa muda mrefu bila kuzolewa.

“Ni aibu manispaa kuongeza viwango vipya vya tozo bila uboreshaji wa soko, baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wanashindwa kuingiza bidhaa zao kutokana na uchafu hivyo hurudia nje,” alisema mfanyabiashara mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Karua.

MWENYEKITI SOKONI ANENA
Alipoulizwa Mwenyekiti wa Wafanyabiashara, Said Habib Kondo alikiri kuwepo kwa hali ya uchafu sokoni hapo.
“Ni kipindi kirefu nimekuwa nikiwaambia manispaa kuboresha soko, wanasema wanataka kulijenga upya, sisi kama viongozi wa wafanyabiashara wa soko hatuna fungu, mikakati yetu ni ‘kuwaimbia’ manispaa suala hili,” alisema Kondo.

Fukunyuafukunyua ilipiga hodi kwa Msemaji wa Manispaa ya Ilala, David Sanga na kumuuliza kuhusiana na kero hiyo alikiri kuwepo.“Ni kweli mkandarasi aliyekuwa akikusanya ushuru, kufanya usafi na kusomba taka tuna mgogoro naye hivyo manispaa ndiyo imechukuwa nafasi yake kwa kufanya shughuli zote alizokuwa akizifanya,” alisema.

Kuhusu madai ya marejesho ya asilimia kumi sokoni hapo ili lijihudimie alisema analifuatilia suala hilo.Yeyote mwenye kero au malalamiko awasiliane nasi kwa namba hizo hapo juu.

0 comments:

Post a Comment