Wasiliana Nasi

Wasiliana Nasi

Tuesday, June 2, 2015

MJANE: UKIPATA AJALI UKATOKA SALAMA MSHUKURU MUNGU!


Na Mwandishi Wetu
“SIKUAMINI kama kungekuwa na siku ndoto ya maisha yangu ingebadilika na kufikia hatua hii ya mateso yasiyo na ukomo, kwa sasa shughuli zangu zote zimesimama nimekuwa mtu wa kuishi kwa kuombaomba ndani ya miaka minne”

Luna Hassan Mwampyati aliyekatika mkono baada ya kupata ajali.
Hivyo ndivyo mkazi huyu wa Tandika Azimio, jijini Dar es Salaam, Luna Hassan Mwampyati (34) alivyoanza kuelezea mkasa wa ajali aliyopata na kupoteza kiganja cha mkono wake wa kushoto.
Ajali iliyosababisha mama huyo kupatwa na masaibu hayo, ilihusisha Basi la New Force iliyotokea Januari 28,2012 maeneo ya Nyororo, Mafinga mkoani Iringa.
Akisumulia zaidi, mama huyo anasema:
NILIJIKUTA NIMELOA DAMU
“Nakumbuka siku hiyo ya tukio nilikua nikisafiri kutoka Dar kwenda mkoani Mbeya, nikisafirisha biashara yangu ya vitenge, nilikua nimesinzia, wakati huo ilikuwa saa tisa alasiri. Nikiwa nimekaa kiti namba 28, nilisikia kishindo kikubwa na nilipozinduka ndani ya basi kulikuwa na vumbi basi lilikuwa limepinduka, niligundua mkono umebanwa.
“Katika hali isiyokuwa ya kawaida, kila mmoja alikuwa akilia huku akiomba msaada, mwili wangu ulikuwa umeloa damu yangu na abiria waliokuwa wamejeruhiwa waliokuwa wakilia, hakuna aliyeweza kumuokoa mwenzake, kila moja alitafuta jinsi ya kujinasua.
“Nilijaribu kuvuta mkono wangu lakini ilishindikana, nikawa napata maumivu kupita kiasi, niliomba msaada kwa watu bila mafanikio.Wasamaria wema walipojitokeza, walianza kuchana gari kwa kutumia shoka na mapanga.
MKONO WASAGIKA
“Mkono wangu ulipotolewa ulikua umesagika na vipande vikawa vinaning’inia.
Miili kadhaa ya watu waliopoteza maisha walikuwa wamenilalia, hivyo ikawa vigumu kujinasua.
“Nikiwa katika hali hiyo, mtoto wa miaka kama mitatu hivi aliyekuwa na mama yake, alinikumbatia alifikiri nilikuwa mama yake.
Alipokuwa hospitali baada ya kupata ajali.
“Alikuwa akilia kwa uchungu huku akitoa sauti ‘mama,mama,mama nakufaaa’, alinikumbatia muda wote hadi pale wasamaria wema walipokuja kumbandua kwangu.
MKONO WAKATWA
“Tuliondolewa na kulazwa pembeni mwa barabara, watu walikuwa wakisema kulikuwa na watu watano waliojeruhiwa vibaya, nilisikia kwamba basi letu lilikuwa likijaribu kulipita basi lingine ndipo liligongana na lori uso kwa uso.
“Tulichukuliwa hadi Hospitali ya Makambako kwa bahati mbaya kipindi hicho kulikua na mgomo wa madaktari hapo tukahamishiwa Hospitali ya Misheni ya Ilembula.
“Polisi walikuwa bega kwa bega kuhakikisha tunapata huduma, kesho yake ndugu zangu walifika wakitokea Mbeya baada ya kupata taarifa, walikuta kiganja changu kimeshakatwa.“Niliendelea kupata matibabu, nikapata nafuu lakini mizigo yangu ya vitenge vya biashara yenye thamani ya shilingi milioni moja ilipotea, mtaji ukawa umekatika, sikuwa na jinsi ya kuinuka tena katika maisha, mume wangu alishafariki miaka 15 iliyopita nikawa mama na baba wa watoto wangu watatu.
Ajali iliyomsababishia kupoteza mkono wake.
“Mmoja alikuwa anasoma sekondari aliacha kusoma, nilikosa fedha za kumsomeshea, hali hiyo iliwakuta hata hawa wadogo, nimeshindwa maisha kwa ujumla.“Nyumba niliyopanga kodi ikawa imeisha ilibidi tutimuliwe kutokana na kutokuwa na fedha ya kulipia, nilifikiria mengi sana kwani hata njaa ilitukabili.
“Nilihama pale baada ya chumba kimoja na bibi mmoja, chumba hicho kilitumika kufugia nguruwe awali, nilikisafisha, tukawa tunaishi kwa dhiki kubwa licha ya kusaidiwa na wasamaria wema wachache waliojua historia yetu.
“Hata hivyo, baada ya muda mfupi tukafukuzwa kwa madai kwamba anataka kuifanyia ukarabati kisha aiuze.
“Hapo ndipo nilipatwa na majonzi huku nikifikiria pa kwenda, sikuweza kupata majibu kwa urahisi, baadaye nikahamia Tandika kwa mdogo wangu anayeendesha maisha yake kwa kuuza mbogamboga, akikosa tunalala njaa.
“Kwa sasa bado sijapona vizuri kwani wakati wa baridi napata maumivu makali. Sina biashara yoyote, kazi yangu ilikuwa ni biashara ya vitenge na saluni, nimepata pigo kubwa sana na familia yangu nayo imeathirika.
Akiwa na familia yake kabla ya kupata ajali.
“Nawaombeni Watanzania wenzangu mnisaidie nipate mtaji ili niweze kufanya biashara ambayo naamini itaniwezesha kuendesha maisha na kuacha kuombaomba jambo ambalo silipendi isipokuwa nalazimika kufanya hivyo kwa sababu ya shida,” alisema mama huyo.Kwa yeyote atakayeguswa na kilio chake awasiliane naye kwa namba 0763 224986 au 0656 238087- Mhariri

0 comments:

Post a Comment