Wasiliana Nasi

Wasiliana Nasi

Thursday, February 26, 2015

MWANDISHI ALBINO ANUSURIKA KIFO MARA MBILI

OJUKU ABRAHAM/Amani

MWANDISHI wa habari mwandamizi, Henry Mdimu ambaye ni Albino, aliyejiteua kuwa Balozi wa kuwatetea walemavu wa ngozi kwa kuanzisha kampeni aliyoiita Imetosha, kutokana na kukithiri kwa mauaji dhidi yao, amesema alinusurika kuuawa mara mbili na watu alioamini walihitaji viungo vyake, Amani lina data kamili.

Mwandishi wa habari mwandamizi, Henry Mdimu.

Akizungumza na gazeti hili juu ya nia yake hiyo ya kujitolea kupinga mauaji hayo anayotegemea kuwatumia zaidi wasanii wa muziki wa kizazi kipya ili wapaze sauti zao, alisema siku zote hakuwahi kudhani kama tishio hilo ni kubwa na hata aliponusurika mara ya kwanza akiwa mkoani Dodoma, bado hakuamini.

“Nilikuwa Dodoma natoka muziki usiku, nikachukua teksi ili inirudishe hotelini nilikofikia, mara ndani ya teksi wakapanda watu wengine wawili, sikujali nikajua ni mashanta, sasa nikashangaa mwelekeo wa gari ni tofauti na nilivyowaelekeza, nikaanza kubishana nao. Nilivyoona hivyo, nikampigia simu rafiki yangu niliyemuacha disco, nikaiacha simu wazi ili asikie kinachoendelea ndani ya gari, baadaye nikamwambia nipo maeneo ya stendi, akaniambia anakuja.

“Sasa tukawa tumesimama tunabishana, mara rafiki yangu akatokea akiwa na mtu mwingine, wakasaidiana kunishusha nikaendelea na safari zangu,” alisema Mdimu, baba wa mtoto mmoja, ambaye pia ni blogger.

Tukio la pili lililohatarisha maisha ya mwandishi huyo, ambaye pia amewahi kufanya kazi Global Publishers, ambalo analielezea kuwa ndilo lilikuwa hatari zaidi, lilimtokea mkoani Mbeya, alikokuwa amekwenda kwa shughuli zake za kikazi na kufikia katika hoteli moja ambayo ameisahau jina.

“Nilikuwa chumbani kwangu nikapigiwa simu na mapokezi wakaniambia kuna wageni wako. Nikatoka na kuwakuta watu ambao siwajui, waliojitambulisha kama mashabiki wangu wanataka tuongee.

Basi tukakaa sehemu ya kinywaji tukaanza kupata, sasa kumbe ikawa kila nikienda chooni kujisaidia, wao wanajifanya kuzungumza ili kuwazuga watu eti kwamba mimi ni mtu wa Mbeya lakini nakataa kwenda kwetu na hawajui watanishawishi vipi ili siku hiyo niondoke nao,” alisema.

Mdimu alisema mara ya mwisho alipokwenda chooni, mmoja wa wahudumu alimfuata na kumwambia akirudi mezani asinywe kinywaji chake kwa sababu wale watu waliweka kitu kibaya, jambo lililomtisha na kuwaomba wawaite polisi ambao walikuja na kuwakamata watu hao ambao walishindwa kujieleza. “Waliwachukua na kuondoka nao, sikuwahi kufuatilia kilichoendelea,” alisema Mdimu na kuongeza kuwa mauaji ya hivi karibuni ya mtoto huko Geita, yamemfanya sasa kutambua hatari kubwa iliyo mbele yao na kuomba jamii kuungana ili kuwaangamiza wahalifu hao.

0 comments:

Post a Comment