Wasiliana Nasi

Wasiliana Nasi

Tuesday, February 10, 2015

FAMILIA KUTEKETEA KWA MOTO SIMULIZI YAKE INATISHA!

Na Haruni Sanchawa/Uwazi

SIMULIZI ya vifo vya watu sita wa familia moja waliopoteza maisha kwa ajali ya moto huko Kipunguni jijini Dar es Salaam wiki iliyopita inatisha, baada ya majirani kuanika ushuhuda waliousikia dakika chache kabla ya wapendwa hao kukata pumzi, Uwazi lina habari kamili.
Nyumba iliyoteketea kwa moto na kusababisha vifo vya watu sita.

Katika ajali hiyo, Kapteni mstaafu wa JWTZ, David Mpira, mkewe, watoto wao na wajukuu wawili walifariki kwa moto huo unaodaiwa kutokea kutokana na hitilafu ya umeme.

Jirani mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Abdallah Ally alisema siku ya tukio kulikuwa na tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara.“Kwa kweli sijawahi kuona pigo kubwa kwa familia kama hili, huyu ni jirani yetu aliyeishi nasi kwa upendo wa hali ya juu kabisa. Tofauti na inavyofahamika kuwa wanajeshi ni wakorofi, marehemu alikuwa mfano wa kuigwa kwani alikuwa ni mnyenyekevu,” alisema Abdallah.


Waombolezaji wakiwa na simanzi kubwa.

“Jirani yangu ameungua kama kuni, siamini kama hatunaye tena, kweli jamani watu wazuri hawadumu, huyu baba na familia yake walikuwa mstari wa mbele katika masuala ya kijamii,” alisema jirani mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Julius.

Kwa pamoja, majirani hao walisema walipofika eneo la tukio baada ya kusikia vilio kutoka ndani ya nyumba hiyo, walijitahidi kuvunja milango na madirisha, lakini moshi mkubwa ulikuwa umeshatanda ndani.

“Nilisikia sauti ya mama mara tatu akisema Yesu, Yesu, Yesu, hivyo nguvu zetu zote zikaelekea upande uliotoka ile sauti, tukiamini wote watakuwa sehemu moja, lakini kibaya moshi ulikuwa mkubwa sana hivyo ulituzidi nguvu waokoaji ukizingatia hatukuwa na zana za kisasa za uokoaji,” alisema jirani mmoja.

Mashuhuda hao walidai baada ya sauti ya mama huyo kunyamaza, hawakusikia tena chochote hadi baada ya nyumba kuteketea, walipowakuta wanandoa hao maiti zao zikiwa zimekumbatiana mlangoni.
Walioteketea katika ajali hiyo ni David Mpira (60), Selin Egela (50) (Dada wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi Maalum, Prof. Mark Mwandosya, Lucas Mpira (20), Celina Emmanuel (9) na Pauline Emmanuel (4).

Gari la polisi likiwa eneo la tukio.

Mwanafamilia mwingine, Emmanuel Mpira ambaye ni mgonjwa, alikuwa amejilaza nje kwa sababu ya kukimbia joto wakati moto huo ulipoanza na kuwateketeza wenzake. Emmanuel alisema kwamba akiwa amelala nje aliuona moto wa ajabu ukiwaka akaanza kupiga mayowe ya kuomba msaada.

Wananchi mbalimbali waliohojiwa kuhusiana na ajali hiyo, walililaumu Shirika la Umeme la Tanesco kwa kitendo chake cha kuwasha na kuzima umeme kuwa ndicho kilikuwa chanzo kikubwa cha moto huo.

0 comments:

Post a Comment