Wasiliana Nasi

Wasiliana Nasi

Friday, January 16, 2015

TUHUMA NZITO: MAMA AMCHARANGA VIWEMBE MWANAYE

Stori: Gabriel Ng’osha na Denis Mtima/Ijumaa
Unyama wa kutisha! Mama mzazi aliyetajwa kwa jina la Feromena, mkazi wa Meko-Mtongani, Kunduchi jijini Dar, anatuhumiwa kumcharanga viwembe mwanaye wa kumzaa aliyetajwa kwa jina moja la Zena mwenye umri wa miaka kumi.

Mtoto anayefahamika kwa jina la Zena anayedai kunyanyaswa na mama yake.

Tukio hilo la kulaaniwa lilijiri Jumanne wiki hii nyumbani kwa mwanamke huyo maeneo hayo ambapo mama huyo inadaiwa alimsulubu mwanaye huyo anayesoma darasa la nne katika Shule ya Msingi Mtakuja.


Sehemu ya majeraha ya viwembe kichwani kwa mtoto Zena.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, mama huyo alidaiwa kumfungia ndani mwanaye huyo na kuanza kumpa kipigo cha mbwa mwizi.Walidai kwamba ukiachana na siku hiyo, mama huyo amekuwa akimsulubu mwanaye huyo mara kwa mara kwa kumcharanga viwembe na vitu vyenye ncha kali hivyo kumwachia majeraha sehemu mbalimbali za mwili.
Sehemu ya majeraha yaliyo mgongoni mwa zena.

Mjumbe wa mtaa huo aliyejitambulisha kwa jina la Elizabeth Mziga alikiri kupokea malalamiko kutoka kwa majirani juu ya unyanyasaji na uteswaji wa mtoto Zena.Mjumbe huyo alisema kuwa tuhuma hizo alishazifikisha polisi ambapo mama huyo alikamatwa lakini baada ya muda alionekana akidunda mtaani kama kawa.

Mama mzazi wa mtoto Zena,Bi.Feromena akibanwa kwa maswali.

Baada kujazwa habari na majirani na mjumbe huyo, kile kikosi kazi cha Oparesheni Fichua Maovu cha Global Publishers kiliingia mzigoni ambapo kilianza kwa kumsaka mtoto huyo na kuzungumza naye.
Alipopatikana, mtoto Zena alieleza namna mama yake alivyokuwa akimfanyia matendo ya kinyama huku akimnyima haki ya msingi ya kwenda shule.
Mama Zena, Bi. Feromena akiwa chini ya ulinzi.

Alisema mama yake amekuwa akimtuhumu kumwibia fedha zake na kwenda kutumia shuleni hivyo hakupaswa kurudi tena shuleni na kuongeza kuwa siku ambazo alikuwa akilala kwa amani ni zile ambazo alikuwa ametoroka nyumbani na kwenda kulala kwa majirani.


Wananchi wakishuhudia mkasa huo wa kusikitisha.

OFM ilishuhudia mwili wa Zena ukiwa na makovu na kuvimba huku akidai kuwa aliunguzwa na ‘frampeni’ (kikaangio) hasa sehemu za kiunoni na mgongoni.Alisema mama yake alimtishia kuwa endapo atamwambia baba yake atakiona cha mtema kuni.

“Jamani mama amekuwa akinipiga na kunikata viwembe bila kuniambia kosa langu. Naombeni msaada nateseka,” alisema Zena kwa masikitiko makubwa.OFM, kwa kwa kushirikiana na mjumbe wa eneo hilo walikwenda kuripoti tukio hilo kwenye Kituo Kidogo cha Polisi cha Mtongani lakini hakukuwa na dawati la jinsia hivyo polisi walikwenda kumkamata mama huyo kwa ajili ya kumpeleka kituo kikubwa.
Moja ya wazee akionesha jalada la kesi aliyofunguliwa mama zena.

Kwa upande wake mama huyo alipoulizwa sababu hasa ya kumsulubu mwanaye alisema si kweli bali anachojua ni siku moja aliyompiga baada ya kuchukua fedha zake na kwenda kununulia maandazi.
“Sijui aliyemkatakata viwembe,” alisema mama Zena kwa kifupi.

Baada ya kufikishwa kwenye kituo kikubwa cha Polisi cha Kawe, mama huyo alifunguliwa jalada la kesi namba KW/RB/439/015-SHAMBULIO LA KUDHURU MWILI hivyo anasubiri kufikishwa kwenye mkono wa sheria.

0 comments:

Post a Comment