Wasiliana Nasi

Wasiliana Nasi

Wednesday, October 1, 2014

MATATIZO YA UGONJWA WA MOYO WA KUZALIWA (CONGENITAL HEART DISEASE) -2




Wiki iliyopita tulikuwa tumeanza kuzungumzia juu ya matatizo ya moyo ya kuzaliwa sehemu ya kwanza, leo tunaendelea sehemu ya pili na ya mwisho.Vilevile sababu nyingine inayoweza kufanya mtoto azaliwe na matatizo ya moyo ni ugonjwa wa kisukari kwa mama wakati wa ujauzito.

Leo tuangalie tatizo la mtoto kuzaliwa na tundu katika kuta za juu za moyo au Atrial Septal Defect (ASD).
Wakati kijusi (fetus) kinapoendelea kukua, kuta kati ya atria mbili za moyo inayoitwa kitaalamu interatrial septum nayo pia hukua ili kutenganisha chemba ya kulia na kushoto.

Lakini katika kipindi hiki huwa kuna tundu kati ya kuta hizo linaloitwa foramen ovale. Tundu hili ni la kawaida kwa kipindi hiki cha kijusi na husababisha damu yenye oksijeni kutoka kwenye kondo la nyuma (placenta) kutokwenda kwenye mapafu ambayo bado hayajakomaa na kuelekea sehemu nyingine za mwili hasa kichwani.

Kipande cha tishu kinachoitwa kitaalamu septum primum hufanya kazi kama valvu katika tundu hilo. Mara tu mtoto anapozaliwa, shinikizo katika mishipa ya damu ya mapafu (pulmonary circulatory system) hushuka na kusababisha tundu hilo kufunga kabisa.

Iwapo tundu hilo halitafunga wakati huu mtoto huzaliwa akiwa na tundu katika moyo. Tundu hilo huwa halifungi kabisa kwa karibu asilimia 25 ya watu, hivyo pindi shinikizo la damu linapoongezeka katika mishipa ya damu ya mapafu kutokana na sababu mbalimbali, au kutokana na matatizo ya kikohozi cha muda mrefu, husababisha tundu la foramen ovale kutofunga na kubakia wazi.

Tatizo hili hutokea kwa mtoto mmoja katika kila watoto 1,500 wanaozaliwa. Lakini kwa kuwa pindi mtoto anapozaliwa huwa hakuna dalili zozote za tatizo, mara nyingi huwa haligunduliki mapema hadi pale anapokua.

Zipo aina kuu 6 za tundu katika kuta za juu za moyo lakini aina ya Ostium secundum hutokea kwa wingi, na huchangia kwa asilimia 6 hadi 10 ya magonjwa yote ya moyo ya kuzaliwa nayo. Tatizo hilo hutokana na ukubwa wa tundu la foramen ovale na kutokukua vyema ukuta unaoitenganisha. Hata hivyo, karibu asilimia 70 ya watu wenye tatizo hili huweza kufikisha miaka 40 ndipo dalili huanza kujitokeza.

Katika baadhi ya nchi zilizoendelea kama Marekani watoto wote wanaozaliwa hupimwa ili kuona kama wana tundu katika mioyo yao, na wale wanaopatikana na tatizo hilo hufanyiwa matibabu ya upasuaji na kurekebishwa tatizo hilo.

Itaendelea wiki ijayo.

0 comments:

Post a Comment