Wasiliana Nasi

Wasiliana Nasi

Wednesday, October 15, 2014

UGONJWA WA TUNDU KATIKA MOYO KWA WATOTO




Kama kawaida safu hii huwa tunajadili masuala mbalimbali yanayohusu afya na tiba ili kupata ufahamu zaidi juu ya kuimarisha afya zetu na ya jamii kwa ujumla.
Leo tutazungumzia ugonjwa unaojulikana kama tundu katika kuta za ventrikali za moyo au kwa kitaalamu Ventricular Septal Defect (VSD).

Tatizo hili hutokea mara nyingi ambapo watoto 2-6 kati ya 1,000 uzaliwa nalo.
Tundu katika kuta za chini za moyo au VSD ni pale panapokuwepo na uwazi katika sehemu ya kuta ya septum inayotenganisha chemba za ventrikali zilizo chini ya moyo.

Moyo unapoanza kuumbika huanza kama bomba lililo wazi na kuendelea kujigawa katika sehemu mbalimbali na kuunda kuta.
Iwapo kitendo hicho hakitatekelezwa ipasavyo, hutokea uwazi katika kuta ya septum kwenye chemba za chini.

Kuwepo tundu hilo huruhusu damu yenye oksijeni kupita kutoka chemba ya kushoto ya chini ya moyo na kuingia katika chemba ya kulia ya chini ya moyo, badala ya kuingia kwenye mshipa wa aorta na kuelekea nje ya moyo kama inavyotakiwa.

Tundu la VSD linaweza kuwa dogo, la kati au kubwa. Tundu dogo katika kuta za chini za moyo huruhusu damu ndogo tu kutoka upande mmoja wa moyo kwenda wa pili hivyo haliathiri utendaji wa kawaida wa moyo na kwa kawaida huwa halihitaji matibabu maalumu.

Matundu ya aina hiyo huziba yenyewe wakati moyo unapoendelea kukua kipindi cha utotoni. Matundu yenye ukubwa wa kati na kubwa katika kuta za chini za moyo huruhusu kiwango kikubwa zaidi cha damu kupenya toka upande mmoja wa moyo kwenda mwingine, na mara nyingi huhitaji matibabu maalumu.

Watoto wenye tundu dogo katika moyo, huweza kukua bila matatizo yoyote, wakati wale wenye tundu kubwa huanza kuonyesha dalili mapema.

Vifuatavyo ni vihatarishi ambavyo vinaweza kusababisha mtoto kuzaliwa na tundu katika kuta za chini za moyo. Mama kuwa na maambukizi ya Rubella katika kipindi cha ujauzito au kuwa na ugonjwa wa kisukari cha wakati wa ujauzito ambao haujadhibitiwa na kuwa mnywaji wa pombe au mtumiaji wa madawa ya kulevya.

Mjamzito akitumia bila ushauri wa daktari baadhi ya dawa za hospitali katika kipindi cha ujauzito pia huweza kusababisha mtoto azaliwe na tundu katika kuta za chini za moyo.

DALILI
Iwapo tundu ni dogo huwa halina dalili yoyote na pale mtoto anapoendelea kukua tundu hilo hujifunga lenyewe. Lakini tundu likiwa kubwa, japokuwa mtoto anayezaliwa huwa haonyeshi dalili yoyote katika kipindi hicho lakini baadaye huwa na dalili zifuatazo.

Rangi ya ngozi yake, midomo na kucha hubadilika na kuwa ya bluu, kunyonya au kula huwa kwa shida sana, ukuaji na kupumua kwa shida, kuchoka haraka, kujaa miguu na kuvimba tumbo, kuwa na mapigo ya moyo ya haraka.

Mtoto mwenye tatizo hili anapopimwa na daktari kwa kifaa, huweza kusikia ishara ya ongezeko la sauti ya ziada ya mapigo ya moyo wa mtoto hali ambayo kitaalamu huitwa holosystolic murmur.

Itaendelea wiki ijayo.

0 comments:

Post a Comment