Wasiliana Nasi

Wasiliana Nasi

Tuesday, October 21, 2014

UGONJWA WA TUNDU KATIKA MOYO KWA WATOTO-2




MADHARA YA TUNDU KATIKA MOYO
Madhara ambayo yanaweza kusababishwa na tundu katika kuta za chini za moyo ni Eisenmenger syndrome, hali ambayo hutokea pia pale mtu anapokuwa na tundu katika kuta za juu za moyo.
Tatizo hili hutokea wakati mtiririko wa damu unapoongezeka kutoka kushoto kwenda kulia kupitia tundu katika kuta za moyo, suala ambalo huongeza mtiririko wa damu katika mishipa ya mapafu na kusababisha shinikizo la damu katika mapafu.

Hali hii husababisha ongezeko la shinikizo la damu katika upande wa kulia wa moyo na kubadilika kwa shanti kutoka kulia kwenda kushoto.

Matokeo yake ni kuwa damu isiyo na oksijeni iliyotakiwa kwenda kwenye mapafu kwa ajili ya kusafishwa huchanganyika na damu yenye oksijeni iliyoko upande wa kushoto na kusambaa mwilini.
Madhara mengine ya tundu la VSD ni kupata ugonjwa wa kiharusi, moyo kushindwa kufanya kazi vizuri pia maambukizi katika kuta za ndani za moyo (endocarditis) ugonjwa ambao tutauelezea katika matoleo yajayo.

Akinamama waliozaliwa na tatizo hili, ambao wametibiwa na hawakupata madhara wanaweza kushika mimba na kupitisha kipindi cha ujauzito bila matatizo yoyote.
Isipokuwa wale ambao hawakutibiwa au ambao tayari wameshapata madhara, hushauriwa kutoshika ujauzito kwa sababu ya hatari zinazoweza kutokea katika kipindi cha ujauzito.
Vilevile kwa akinamama waliozaliwa na tatizo hili, uwezekano wa watoto wao kuzaliwa na tatizo hili huwa mkubwa.

TIBA
Inafaa kujua kuwa, karibu nusu ya wagonjwa wenye tatizo hili huwa hawahitaji matibabu ya aina yoyote ile kwa kuwa tatizo hili hujirekebisha katika miaka ya mwanzo ya maisha yao.
Hata hivyo, kwa wale ambao watahitaji matibabu, hutibiwa kwa dawa au upasuaji kwa kutegemea ukubwa wa tatizo lenyewe.

Dawa zinazotumika kutibu ugonjwa huu ni zile ambazo hupunguza kasi ya moyo, huongeza nguvu ya mapigo ya moyo na zile ambazo hupunguza maji mwilini au diuretics.
Utaratibu wa kuziba tundu umegawanyika katika sehemu mbili na hufanyika iwapo tundu ni kubwa sana, au halikujirekebisha lenyewe wakati mtoto alipokuwa anakua na pale ikiwa dawa alizopewa mgonjwa hazikusaidia.

Pale inapohitajika upasuaji, mgonjwa hufanyiwa oparesheni ambapo kifua hufunguliwa ili kuziba tundu la VSD.

Matibabu mengine ni kupitisha mrija katika mshipa wa damu hadi katika sehemu ya tatizo kwenye moyo na kuliziba kwa kutumia kifaa maalumu. Kwa njia hii, huwa hakuna haja ya kufanya upasuaji wa kufungua kifua cha mgonjwa.

MWISHO

0 comments:

Post a Comment