Wasiliana Nasi

Wasiliana Nasi

Monday, December 1, 2014

SIKU YA UKIMWI DUNIANI; MKOA WA NJOMBE BADO UNAONGOZA KWA MAAMBUKIZI




Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), Dkt. Fatma Mrisho akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu Kauli Mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani isemayo, Tanzania Bila Maambukizi Mapya ya VVU, Vifo Vitokanavyo na Ukimwi na Ubaguzi na Unyanyapaa inawezekana inayolenga kupunguza maambukizi Mapya ya Ukimwi, kupunguza vifo vitokanavyo na Ukimwi na kukomesha vitendo vya unyanyapaa kwa asilimia Sifuri.

LEO ni Siku ya Ukimwi Dunia ambapo Kitaifa maadhimisho hayo yanafanyika mkoani Njombe. Kwa takwimu zilizotolewa na Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) 2011/12, Mkoa wa Njombe, Mbeya na Iringa ni vinara wanaoongoza kwa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi nchini huku Pemba na Unguja zikiwa chini kwa maambukizi hayo.



Mkoa wa Njombe unaongoza kwa maambukizi ukiwa na asilimia 14.8, ukifuatiwa na Iringa yenye maambukizi asilimia 9.1 na Mkoa wa Mbeya unashika nafasi ya tatu kwa asilimia 9.

Mikoa mingine na asilimia za maambukizi katika mabano ni Shinyanga (7.4), Ruvuma (7.0), Dar es Salaam (6.9) Rukwa (6.2), Katavi (5.9), Pwani (5.9),Tabora (5.1), Kagera (4.8) na Geita (4.7).

Mikoa mingine aliyoitaja ni Mara (4.5), Mwanza (4.2), Mtwara (4.1), Kilimanjaro (3.8), Morogoro (3.8), Simiyu (3.6), Kigoma (3.4), Singida (3.3), Arusha (3.2), Dodoma (2.9), Lindi (2.9), Tanga (2.4), Manyara (1.5), Unguja (1.2) na Pemba (0.3).

Nchi nzima, asilimia 5.1 ya wanawake na wanaume wenye miaka 15-49 wana maambukizi ya VVU. Wanawake wana kiwango kikubwa cha maambukizi kuliko wanaume mijini na vijijini. Asilimia 7.2 ya wakazi wa mijini wana maambukizi ya VVU ukilinganisha na asilimia 4.3 ya wakazi wa vijijini.

Katika takwimu hizo, Watanzania walioonesha kuwa na ufahamu sahihi wa elimu kuhusu Virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi wanafikia asilimia 60 jambo linalosababisha kuwepo mwamko mdogo wa kubadili tabia.

Kuhusu tohara kwa wanaume, takwimu zilionyesha inapunguza maambukizi ya Ukimwi kwa asilimia 60 na kusisitiza kuwa ipo haja ya kutoa elimu zaidi juu ya uelewa wa ugonjwa huo.

Visababishi vya Ukimwi:
Miongoni mwa vipengele muhimu ni pamoja na vifuatavyo:
-Uasherati
-Matumizi madogo na yasiyo endelevu ya kondomu
-Ngono za marika yanayotofautiana sana
-Kuwa na wapenzi wengi.
-Ukosefu wa elimu ya maambukizo ya UKIMWI
-Kuwepo kwa maradhi mengi ya ngono kama vile tutuko, homa,
-Jando kwa wanaume
-Sababu za mahali husika, za kushamiri kwa janga nchini ni:
-Umaskini na biashara ya ngono pamoja na ongezeko la wafanyabiashara wa ngono
-Tabia mbaya za ngono za wanaume kutokana na kuruhusiwa kimila kuwa na nguvu
-Kukosekana usawa wa kijamii, kiuchumi, kisiasa na kijinsia pamoja na unyanyaswaji wa wanawake na wasichana walio ndani na nje ya mahusiano.
-Matumizi ya pombe na dawa za kulevya.
-Tabia za kimila (kama vile utakasaji wajane na jando na unyago)
-Safari za aina zote zinazosababisha kuwa mbali kwa wanandoa na ongezeko la mahawara
-Kutokutahiriwa

0 comments:

Post a Comment