Wasiliana Nasi

Wasiliana Nasi

Tuesday, November 11, 2014

MAMA: AWALI NILIJUA NINA UJAUZITO KUMBE SIYO

Stori: Na Makogoro Oging’
Mama mmoja mkazi wa Kijiji cha Kipanga, Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, Flora Samweli Luvinga (24) hali yake ipo hatari baada ya kuvimba tumbo na kumsababishia maumivi makali.“Awali nilidhani ni mimba baadaye nikajua kuwa kumbe siyo bali ni ugonjwa ambao unanipa mateso kwa muda mrefu, sasa sijui hatima ya maisha yangu hapa duniani,” alisema Flora.


Flora Samweli Luvinga (24) anyesumbuliwa na uvimbe mkubwa tumboni.

Mgonjwa huyo ambaye kuumwa kwake kumechukua muda mrefu bila mabadiliko ya kupata nafuu, afya yake imezidi kudhoofu jambo lililomfanya mama yake mzazi kupatwa na presha siku za hivi karibuni na kufariki dunia baada ya kushindwa kupata fedha kwa ajili ya kumtibia.

Katika mahojiano na mwandishi wa habari hii wiki iliyopita saa chache baada ya kurejea jijini Dar akitokea Iringa, Flora aliyekutwa amekaa chini maeneo ya Mwenge akipumzika kutokana na maumivu makali, alikuwa na haya ya kusema:

“Siamini kama ipo siku nitapona na kurejea hali yangu ya kawaida, hapa nilipofikia nimekata tamaa, kwani nimehangaika kwa muda mrefu katika matibabu bila kupata nafuu.
“Ugonjwa wangu ulisababisha mama yangu kukatisha maisha. Nimekuwa nikiwapa shida ndugu zangu, wanashindwa kufanya shughuli zao kwa ajili yangu.”


Flora Samweli Luvinga akiuguzwa na Ndugu yake, Selina Samweli.

HISTORIA YA UGONJWA
Flora alielezea historia ya kuumwa kwake alisema: “Mwishoni mwa Desemba, mwaka 2012 nilianza kusikia maumivu makali tumboni, nikafikiri ni vidonda vya tumbo, nilipata mimba nikajifungua kichanga cha miezi saba katika Hospitali ya Mwananyamala lakini kwa bahati mbaya mtoto akafariki.
“Baada ya muda tumbo likawa linakua, nilifikiri nimepata mimba nyingine lakini cha ajabu nilisikia maumivu kifuani, yalishuka hadi tumboni,wakati huo tulikuwa tukiishi na mume wangu Tandale hapa Dar.

“Ingawa tumbo liliendelea kukua lakini nilipata maumivu makali sana, nilihisi mtoto ambaye ningemzaa angekuwa na matatizo.

TIBA MUHIMBILI, MUME AKIMBIA
“Ilibidi mume wangu anipeleke Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, ili kujua tatizo ni nini na kupata tiba, wakati huo tayari nilikua na watoto wawili. Nikawa sipati unafuu, mume wangu akanikimbia, nikawa sina fedha kwa ajili ya matibabu na kuwanunulia chakula wanangu. “Maisha yalizidi kuwa magumu hali iliyomfanya mama kuuza mazao yake yote na kuja hapa Dar kuniuguza, hata hivyo, aliishiwa fedha.
Flora Samweli Luvinga akisaidiwa na Ndugu na majirani zake.

“Maisha yetu yalizidi kuwa magumu hata chakula kikawa kupata ni shida, tuliishi kwa kusaidiwa na majirani, mama aliamua kwenda Iringa. “Dada yangu aitwaye Selina Samweli alitoka Makambako alikoolewa na kuja kunichukua baada ya mama kumpa taarifa kuhusu jinsi ninavyoumwa.

KODI YA NYUMBA IKAISHA
“Nilimwambia dada sina fedha ya matibabu wala ya kununulia chakula huku kodi ya nyumba nayo ikiwa imeisha.

“Akanihamisha Dar, nikawa naishi naye huko Makambako, nilikua nikipata matibabu katika zahanati ya hapo bila mafanikio, daktari alishauri nipelekwe Hospitali ya Rufaa ya Mbeya. Nilienda.
Tulikaa huko kwa siku 18, tumbo liliongezeka, hakukua na unafuu.

JINSI MAMA ALIVYOAGA DUNIA
Dada naye akawa amechoka alinichukua na kunirudisha kwa mama, tulipofika, mama alitokwa machozi, aliona hali yangu si ya kupona. “Mama hakuchukua muda mrefu, alipatwa na presha, akafariki dunia, nililia sana kwa sababu alinipenda sana, nilibaki nyumbani kwetu peke yangu, nilichukuliwa na dada Selina tukawa tunaishi naye kwake Makambako.

“Aliishiwa fedha akawa anaelekea kukata tamaa, shemeji yangu alishauri niletwe huku Muhimbili, aliomba msaada kwa watu, tukapata nauli ya kuja hapa Dar.
“Hapa unaniona nimekaa, nimetoka Makambako, napumzika, hali yangu imezidi kuwa mbaya, nikipata nafuu nitapelekwa Muhimbili,” alisema Flora.

SINA UWEZO WA DAWA ZA SHILINGI LAKI MBILI
Mwishoni mwa wiki iliyopita mwandishi wa habari hii aliwasiliana naye kwa njia ya simu akiwa Muhimbili kumjulia hali ambapo alisema kwamba tayari amepata baadhi ya vipimo na kimojawapo majibu yamepatikana.

“Natakiwa kununua dawa za shilingi laki mbili. Nimeambiwa hospitali haina dawa hizo, bado nasubiri majibu mengine wiki hii.“Hapa Muhimbili nimetolewa maji tumboni lita sita lakini bado sijaambiwa kinachonisumbua, natarajia kupata majibu wiki ijayo (wiki hii).

“Nawaomba Watanzania wenye moyo wa huruma wanisaidie fedha ya matibabu na chakula kupitia namba hii 0756 613148 au 0657 908261,” alisema mgonjwa huyu akitokwa na machozi.

0 comments:

Post a Comment