Wasiliana Nasi

Wasiliana Nasi

Wednesday, September 24, 2014

UGONJWA WA MOYO WA KUZALIWA (CONGENITAL HEART DISEASE) UNAVYOLETA SHIDA KWA BINADAMU



Leo tutajadili baadhi ya matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo, yaani Congenital Heart Disease.

Magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo ni mengi, kuanzia yale yanayosababishwa na matatizo madogomadogo ambayo kwa kawaida huwa hayaonyeshi dalili au kuathiri maisha ya kawaida ya mtu, hadi yale makubwa yanayohitaji kutibiwa kwa haraka.

Mara nyingi matatizo ya moyo ya kuzaliwa ni yale yanayozuia mtiririko wa damu katika moyo au kwenye mishipa ya damu, au kusababisha damu ipite njia nyingine isiyokuwa ya kawaida kwenye moyo.

Matatizo mengine ya moyo ya kuzaliwa lakini yasiyotokea sana ni pale baadhi ya chemba za moyo zinapokosekana au badala ya kuwepo chemba mbili mtoto huzaliwa na chemba moja ya ventricle au wakati mwingine upande wa kulia au wa kushoto wa moyo huwa haujaumbika kwa ukamilifu hali ambayo kitaalamu huitwa hypoplastic heart.

Miongoni mwa sababu zinazosababisha watoto kuzaliwa na matatizo ya moyo ni pamoja na mmoja kati ya wazazi kuwa na tatizo la moyo la kuzaliwa. Iwapo mama alikuwa na tatizo la moyo la kuzaliwa kuna uwezekano wa asilimia 2.5 hadi 18 wa kuzaa mtoto mwenye tatizo la moyo pia. Iwapo baba alikuwa na tatizo la moyo la kuzaliwa uwezekano wa kuzaliwa mtoto mwenye tatizo la moyo ni kuanzia asilimia 1.5 hadi 3.

Si kawaida mtoto zaidi ya mmoja kuzaliwa na tatizo la moyo katika familia moja. Kuna uwezekano mtoto aliyeko tumboni wakati moyo unapoumbwa akapatwa na maambukizi ya maradhi kama vile rubella, au kuathiriwa na dawa anazotumia mama wakati wa ujauzito au sumu kama vile lithium na hata pombe.

Yote hayo yanaweza kusababisha mtoto azaliwe na matatizo ya moyo. Lakini pia baadhi ya matatizo ya jenetiki huambatana na matatizo kadhaa ya moyo ya kuzaliwa. Matatizo hayo ya jenetiki kitaalamu huitwa Down’s Syndrome, Digeorge syndrome na Turners Syndrome.

Jambo lingine linaloweza kusababisha mtoto azaliwe na matatizo ya moyo ni pale mama anapokuwa na tatizo la kijenetiki linalojulikana kama Phenylketonuria (PKU). Hali hiyo hutokea wakati mwili unaposhindwa kuyeyusha sehemu ya protini inayoitwa phenylalanine (Phe).

Phenylalanine kwa kawaida hupatikana katika kila chakula lakini kiwango chake kinapokuwa juu mwilini huweza kuharibu ubongo na kusababisha mtindio wa ubongo. Baadhi ya wajawazito hupata tatizo hilo ambalo huzidisha uwezekano wa mtoto kuzaliwa akiwa na matatizo ya moyo na ya ubongo pia.

Itaendelea wiki ijayo.

0 comments:

Post a Comment