Wasiliana Nasi

Wasiliana Nasi

Tuesday, August 19, 2014

KAMA WEWE UMEJIFUNGUA SALAMA, MTOTO WAKO NI MZIMA MSHUKURU MUNGU

DUNIANI kuna mengi kiasi kwamba kama mama umebeba ujauzito kwa miezi tisa na kujifungua mtoto salama na mtoto wako ni mzima unapaswa kumshukuru Mungu kwani kuna watu ambao wanapata usingizi wa mang’amung’amu kutokana na mateso ya watoto wao.



Mtoto Godwin Florence Rweyemamu (3) akilia kwa maumivu anayoyapata.

Mtoto Godwin Florence Rweyemamu (3), mkazi wa Kijiji cha Kamala, Kata ya Bangwe mkoani Kigoma yupo ndani ya mateso makubwa yanayomfanya kulia muda wote kutokana na maumivu makali anayoyapata kwa ugonjwa wa kansa unaotafuna macho yake hivyo kumfanya asione.

HISTORIA YAKE
Akizungumza na Uwazi akiwa katika masikitiko makubwa
nyumbani kwa ndugu yake, Manzese jijini Dar, bibi wa mtoto huyo aliyejitambulisha kwa jina la Elda Charles Rweyemamu, mjukuu wake huyo alizaliwa akiwa hana tatizo lolote lakini alipofikisha umri wa miaka miwili na nusu akapatwa na ugonjwa wa mtoto wa jicho upande wa kushoto.

“Tuliamua kumpeleka kwenye Hospitali ya Mkoa wa Kigoma, Maweni ambapo alitibwa akapata nafuu, tukarudi nyumbani.“Lakini wanasema ukizaliwa na balaa ni balaa tu, mwanzo hadi mwisho.


Mtoto Godwin Florence Rweyemamu (3) akiwa na bibi yake, Elda Charles Rweyemamu.

Kwani baada ya muda ugonjwa ulijirudia tena, sasa si mtoto wa jicho ila jicho likaonekana kuwa na uvimbe kidogo. Mimi na mama yake tulishangaa sana, tukaona lazima tuendelee kuhangaika. Tukampeleka katika Hospitali ya Matiazo.

“Madaktari walijitahidi, wakamtibu akapata nafuu tena na uvimbe katika jicho uliisha, tukajua tumeepukana na hilo.

UGONJWA WARUDI KWA KASI
Akiendeleza kusimulia mateso ya mtoto huyo, bibi huyo alisema:
“Baada ya kukaa kwa muda mfupi, ghafla ugonjwa ulirudi tena, sasa eti hata kichwa kilivimba. Hii hali ilitushangaza sana na tukawa tunaulizana ni nini?

“Nilimwambia mama yake kuwa Mungu ni wa kumtumaini muda wote, hivyo tukampeleka tena Hospitali ya Maweni lakini madaktari wakasema ili mjukuu wangu aendelee kuwa na uhai tuje hapa Muhimbili. Tulifunga safari ya kuja ambapo Julai 21, mwaka huu, tukawa tumefika.”

MATUMAINI YAREJEA, YAYEYUKA
“Tulipofika hapa Muhimbili na kuona hospitali yenyewe ilivyo kubwa na madaktari bingwa wengi niliamini kuwa mjukuu wangu angepona na kurudi naye nyumbani akiwa salama lakini cha kushangaza mambo yakawa tofauti na jinsi nilivyokuwa nikifikiria.

”Madaktari walimfanyia uchunguzi, baada ya siku nne waliniambia ugonjwa alio nao huyu mtoto ni kansa.
“Walinitoa machozi zaidi pale waliponiambia kuwa, hata hivyo hawataweza kumtibu kwa vile tulichelewa kumleta.”

“Lakini hata wao waliniambia wakiwa na masikitiko makubwa kwani nilishangaa kuwaona baadhi ya madaktari wakitoa machozi kwa kumuonea huruma mjukuu wangu kwa jinsi anavyolia muda wote kwa maumivu kama unavyomsikia,” alisema.

Aliongeza kuwa, walichofanya madaktari hao ni kumpa dawa ya kutuliza maumivu na kumwambia bibi mtu warudi nyumbani Kigoma kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa yote.

HANA NAMNA YA KURUDI KIGOMA
“Tangu nimeruhusiwa kutoka Muhimbili, Julai 26, mwaka huu sina jinsi ya kurudi nyumbani Kigoma. Nauli hadi kule ni shilingi 70,000. Kwa sasa nimepata hifadhi hapa Manzese kwa mdogo wangu ambaye anaishi kwa kufanya biashara ndogondogo lakini hana fedha. Kuendelea kukaa kwake ni sawa na kero kwani huyu mtoto amekuwa akilia mara kwa mara hali ambayo ni kero kwa wapangaji wenzake.

“Hata chakula ni tatizo, kila siku inabidi nimpeleke katika zahanati kusafisha macho. Kwa muda wa wiki moja nimetumia shilingi 300,000 kwani aliishiwa damu na inabidi aongezwe halafu kuna dawa za kutuliza maumivu aliongezewa, nina shida kubwa sana.”

KWA NINI BIBI NA MJUKUU?
“Kilichonifanya nije mimi huku Dar ni kwa vile mama yake ni mjamzito. Wakati wowote anaweza akajifungua. Pia ana mawazo mengi sana kwani watoto wake wawili, wa kwanza na wa pili walifariki dunia kutokana na magonjwa ya aina mbalimbali na huyu wa tatu ndiyo madaktari wamesema nimrudishe nyumbani tusuburi kifo,” alisema Elda kwa huzuniu

ANACHOOMBA
Anachoomba bibi huyo ni nauli ya kumuwezesha kurudi nyumbani kwake, Kigoma. Kwa aliyetayari anaweza kumsaidia kupitia namba 0762 175 117,
0784 420 215 au 0719 285 100.

Ndugu msomaji, kama ulivyosikia kilio cha bibi huyo ambaye yupo katika wakati mgumu wa kumuuguza mjukuu wake, hebu msaidie kwa chochote ulichonacho, tunaamini Mwenyezi Mungu atakubariki. Mhariri.

0 comments:

Post a Comment