Ndugu zangu, tunapaswa kumshukuru Mungu kwa wema wake anaotufanyia kwa kutulinda sisi tulio hai, hivyo basi jina lake lihimidiwe daima.
Wiki iliyopita tulishuhudia au kusikia tukio la kusikitisha sana wilayani Kahama mkoani Shinyanga ambapo vifo vya watu zaidi ya 45 viliripotiwa baada ya nyumba zao kuanguka kutokana na mvua kubwa ya mawe iliyoambatana na upepo.
Katika tukio hilo lilitokea katika Kijiji cha Mwakata kilichopo Wilaya ya Kahama, tunaelezwa pia watu zaidi ya 90 walijeruhiwa huku wengine wakikosa mahala pa kuishi baada ya nyumba zao kubomoka.
Maafa hayo yametokea siku chache baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kutoa taarifa kuhusu mwelekeo wa mvua za masika mwaka huu.
Taarifa hiyo ilisema hali ya mvua haitarajiwi kuwa ya kuridhisha katika maeneo mengi ya nchi, ingawa ilishawi kuonya uwezekano wa kuwapo mvua kubwa Kanda ya Ziwa.
Kusema kweli hali hii haikutarajiwa na inawezekana kila mtu ameshtushwa na mvua hiyo hasa ikizingatiwa kuwa Mkoa wa Shinyanga ilipo Wilaya ya Kahama ni moja ya maeneo ambayo utabiri wa mwelekeo wa mvua unaonyesha utakuwa na mvua chache mwaka huu.
Jambo muhimu ni Watanzania kulichukulia tukio la Kahama kama msiba unaomgusa kila mmoja. Nachukua nafasi hii kutoa pole kwa wafiwa, lakini juhudi zifanyike kunusuru uhai wa majeruhi na pia kuwasaidia waathirika wengine wa mvua hiyo kubwa.
Binafsi sina nia ya kumnyooshea kidole mtu, taasisi au chombo chochote kuhusu maafa haya ya Kahama, najihisi kuwajibika kwa umma kama Mtanzania ninayeipenda nchi yangu na watu wake, nalazimika kutoa tahadhari kwa serikali na wananchi kwa jumla.
Tahadhari hiyo ni kuhusu namna bora ya kujilinda na majanga mbalimbali yanayotokea nchini ambayo mengi husababisha vifo na wengine kupata vilema vya maisha.
Nchi yetu imekuwa ikikabiliwa na majanga makubwa kama vile mafuriko, ajali za barabarani na matukio ya moto shuleni na kwenye makazi ya watu kwa miaka mingi.
Kinachonisikitisha ni kwamba serikali na hata wananchi, hatuoni kuwapo kwa jitihada madhubuti na mbinu za kuzuia majanga hasa yale yanayoweza kuepukika kama vile mafuriko na moto.
Kwa mfano, matukio ya mafuriko ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara na sehemu mbalimbali nchini, Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania (TMA) aghalabu imekuwa ikiwahi kutoa taarifa za utabiri wa hali ya hewa, ikitahadharisha wananchi kuhusu mvua kubwa zinazoweza kuwa na madhara.
Lakini tujiulize je, taarifa hizi zinafanyiwa kazi na wananchi au wamewahi kuelimishwa kuhusu taarifa kama hizo?
Mara nyingi wakazi wa mabondeni, hasa katika Jiji la Dar es Salaam tumekuwa tukishuhudia wakipuuza ushauri wa wataalamu hao.
Wengi wao wamekuwa na kawaida ya kusubiri janga litokee na kuanza kutapatapa wakiomba msaada.
Kwa upande mwingine, serikali inashindwaje kutumia uwezo wake wa vyombo vya dola kuzuia wananchi wake kukaaa kwenye maeneo hatarishi kama mabonde ambayo ni rahisi kuathiriwa na mafuriko?
Inasikitisha kuona kuwa hata katika masuala yanayohatarisha uhai wa watu, viongozi wanapenyeza siasa. Hatuzui kwani ilishatokea katika Jiji la Dar es Salaam viongozi wa kisiasa wanapishana kauli kuhusu kuwaondoa wananchi waliojenga mabondeni.
Kwa mujibu wa utabiri wa TMA, siku chache zimebaki kabla ya mvua za masika kuanza kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini.
Kutokana na taaarifa hiyo ni wazi sasa ni wakati wa kila mmoja hasa anayeishi mabondeni kuchukua tahadhari ya athari zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua hizo
Inawezekana kabisa kupunguza ukubwa wa baadhi ya athari za majanga kwa kuchukua hatua za tahadhari mapema.
Nitoe wito kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadick kuhimiza kidola juu ya watu wa mabondeni ili yaliyotokea Kahama yasihamie jijini Dar es Salaam.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.
0 comments:
Post a Comment