Askari wa Chad na Niger wakiwa Damasak.
Makumi ya miili ya watu wanaosadikiwa kuuawa na wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri wa Boko Haram, imegunduliwa katika Mji wa Damasak uliopo Kaskazini Mashariki mwa Nigeria.
Taarifa zinaeleza kuwa, miili hiyo ya watu 70 ambayo mingi kati yake imekutwa ikiwa imekatwa vichwa, imegunduliwa na askari wa Chad na Niger katika mji huo wa Damasak nchini humo. Tayari uchunguzi umeanzishwa kwa lengo la kuwatambua wahusika wa ukatili huo, ingawa kidole cha lawama tayari kimeelekezwa kwa wanachama wa kundi la kitakfiri la Boko Haram, ambalo limekuwa likitekeleza mauaji kama hayo.
Hadi siku ya Jumamosi iliyopita, ambapo askari hao wa Chad na Niger waliuvamia mji huo na kuukomboa kutoka kwa wanachama wa kundi la Boko Haram, ulikuwa umetelekezwa kabisa na serikali ya Nigeria.
Tangu mwezi Novemba mwaka jana ambapo mji huo ulidhibitiwa na kundi hilo, wakazi wake walikuwa wakijaribu kutoroka ingawa hata hivyo walikuwa wakizuiliwa na magaidi hao wanaotekeleza jinai kwa jina la Uislamu.
Inaelezwa kwamba, baada ya mji huo kudhibitiwa na kundi hilo, wanachama wake walivamia maduka na makazi ya watu na kupora kila walichokitaka, huku wakiwabaka na kuwanajisi wanawake na wasichana wa mji huo.
CHANZO: BBC NEWZ
0 comments:
Post a Comment