Wasiliana Nasi

Wasiliana Nasi

Wednesday, March 25, 2015

MAAMBUKIZI YA FANGASI SEHEMU ZA SIRI -3

WIKI iliyopita tulieleza madhara ya fangasi zehemu ya siri na jinsi ugonjwa huo unavyosumbua wanawake.
Leo tunaendelea kuelezea fangasi sehemu za siri wanavyosumbua na tuliahidi kwamba tutaeleza tiba yake.
Baada ya kueleza mengi kuhusiana na ugonjwa huu leo tutaeleza matibabu yake ambayo huusisha dawa za kutibu fangasi (antifungal drugs) kama vile dawa za kupaka za Topical Clotrimazole, Topical Nystatin, Fluconazole au Topical Ketoconazole.

Wagonjwa wenye maambukizi yasiyo makali yaani Uncomplicated Vaginal Candidiasis wanaweza kutumia dawa za kupaka (cream) za fangasi kama vile Butoconozale, Miconazole, Clotricomazole nk. Dawa hizi hutumika kwa muda wa siku 3-7 kulingana na aina ya dawa. Mgonjwa anashauriwa kupaka dawa ndani ya uke pamoja na maeneo yote yanayozunguka sehemu hiyo.

Lakini pia mgonjwa anaweza kupewa dawa za kutumbukiza ukeni ambayo atatumia kwa muda wa siku 3-14 kulingana na aina ya dawa. Dawa hizo ni pamoja na Miconazole, Tiaconazole, Terconazole, Nystatin nk.
Kwa wale wenye maambukizi makali yaani Complicated Vaginal Candidiasis, kabla ya kupewa tiba, ni muhimu kwanza kufanyiwa kipimo cha kuotesha sehemu ya uchafu unaotoka ukeni ili kuwa na uhakika kama kweli fangasi wanaosababisha maambukizi haya ni Candida Albicans ama la.

Fangasi wengine aina ya Candida Glabrata pia wanaweza kusababisha aina ya maambukizi haya na huwa siyo rahisi kutibika kwa kutumia matibabu ya kawaida na pia si rahisi kuonekana kwa kutumia hadubini (microscope).

Matibabu ya wagonjwa wenye aina hii ya fangasi hujumuisha matumizi ya dawa za kupaka (cream) au vidonge vya kuweka ukeni kwa muda mrefu, yaani kwa muda wa siku saba hadi kumi na nne.
Wengine hutibiwa kwa dawa aina ya Fluconazole ambayo hutumika kila baada ya siku tatu (yaani siku ya 1, siku ya 4 na siku ya 7). Mara baada ya kumaliza tiba hii, mgonjwa hutakiwa kuendelea nayo mara moja kwa wiki kwa muda wa miezi sita.

Ikiwa matibabu haya hayatasaidia basi mgonjwa anaweza kushauriwa kutumia mchanganyiko wa Fluconazole pamoja na dawa ya kupaka ya Clotrimazole mara mbili au moja kwa wiki kulingana na dozi ya dawa, au Fluconazole na dawa nyingine za kupaka kwa wakati mmoja.

Matibabu ya wagonjwa wenye maambukizi hatari sana yaani severe vaginal candidiasis ambayo kwa kawaida huambatana na dalili za uke kuwa mwekundu, kuvimba, michubuko ya ngozi ya ukeni (excoriation) na kutokea kwa mifereji kama vidonda (fissure formation) huwa ni dawa zozote za kupaka zilizotajwa hapo juu kwa muda wa siku 7 mpaka 14.

Pia anaweza kupewa dawa ya fluconazole ambayo hutolewa mara mbili, ambapo dozi ya pili hutolewa siku ya tatu baada ya kutolewa kwa dozi ya awali.Matibabu ya maambukizi ya fangasi ambayo hayasababishwi na Candida albicans ni dawa za kupaka jamii ya nonfluconazole azole groups kama vile Posaconazole, Voriconazole nk.

Zitolewazo kwa muda wa siku 7 mpaka 14 pamoja na kidonge cha boric acid kwa muda wa siku 14. Mtu mwenye maambukizi haya pia anashauriwa kuonana na daktari bingwa wa magonjwa ya akina mama.

WANAWAKE WAJAWAZITO
Kwa vile maambukizi ya fangasi hutokea sana kwa wanawake wajawazito, hivyo basi wanashauriwa kutibiwa kwa kutumia dawa za kupaka tu kwa muda wa siku 7.Nisisitize hapa kuwa dawa aina ya Itraconazole haipaswi kutumiwa na mwanamke mjamzito au anayekusudia kushika mimba kutokana na sababu za kitabibu.

Dawa ya Ketoconazole haipaswi kutolewa bila ushauri wa daktari kwani ina madhara ya kusababisha ugonjwa hatari wa ini. Maambukizi ya fangasi pia huonekana sana kwa wagonjwa wenye Ukimwi. Tiba ya maambukizi haya ni sawa na tiba ya watu ambao hawana ugonjwa wa Ukimwi.

USHAURI
Hata hivyo, kwa wale wagonjwa wa Ukimwi ambao wanapata maambukizi ya fangasi mara kwa mara wanashauriwa kunywa dawa aina ya fluconzole mara moja kwa wiki kama kinga dhidi ya maambukizi haya au kama njia ya kupunguza fangasi hawa.

0 comments:

Post a Comment