Masanja Mwinamila (44) mara baada ya kufikishwa katika kituo cha Polisi Wilaya ya Nzega Juni 15, 2015.
Mtoto Margreth baada ya kufikishwa Kituo cha Polisi Wilaya ya Nzega usiku wa manane.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, ACP Juma Bwire akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na tukio hilo Juni 16, 2015.
Na Daniel Mbega, Nzega
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi
ya Wilaya ya Nzega leo hii imemhukumu Masanja Mwinamila (44), mkazi wa
Kitongoji cha Kona Nne, Kijiji cha Ugembe II, Kata ya Mwakashanhala,
Tarafa ya Puge wilayani Nzega katika Mkoa wa Tabora kwenda jela miaka 10
kwa kosa la kuteka mtoto mwenye albinism, Margreth Hamisi (6).
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo,
Saraphine Nsana, alitoa hukumu hiyo baada ya mshtakiwa kusomewa shtaka
na kukiri kutenda kosa hilo.
Ilielezwa mahakamani hapo kwamba, mnamo
Juni 15, 2015 majira ya saa 3:00 usiku katika Kijiji cha Ugembe II, Kata
ya Mwakashanhala wilayani Nzega, mtuhumiwa alimteka binti huyo kwa
lengo la kwenda ‘kumuuza’ ili ajipatie fedha (kiasi kimehifadhiwa).
Hii ni mara ya kwanza kwa kesi
inayohusisha utekaji nyara, kujeruhi na mauaji dhidi ya watu wenye
albinism kuchukua muda mfupi zaidi, kwani ndiyo kwanza kesi hiyo ya
Jinai Namba 116/2015 imefikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza na
kutolewa hukumu.
Jitihada za Polisi
Mafanikio ya kukamatwa kwa Masanja
Mwinamila akiwa katika harakati za kutaka kumuuza mtoto Margreth Hamisi,
ambaye ni mpwa wake, yametokana na umakini wa Jeshi la Polisi nchini
ambapo maofisa wake wa Kikosi Kazi cha Taifa waliweka mtego na
kufanikiwa kumnasa mtuhumiwa kabla hajamdhuru mateka wake.
Tukio hilo limefanikisha kuubomoa mtandao
hatari wa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) kwani ni
takriban wiki tatu tu tangu maofisa usalama walipofanikiwa kuwanasa watu
wengine sita wakiwa katika harakati za kuuza mifupa inayodhaniwa kuwa
ya binadamu (albino) mjini Kahama Mei 22, 2015 ambapo tayari
wamekwishafikishwa mahakamani pamoja na wengine watatu waliokamatwa
baadaye.
Matukio hayo mawili makubwa yaliyotokea
katika kipindi hicho yamedhihirisha namna serikali kupitia jeshi hilo na
vyombo vingine vya usalama inavyoshughulikia mitandao hiyo hatari usiku
na mchana ili kuhakikisha Watanzania wote wanaishi kwa amani na
usalama.
Kukamatwa na hatimaye kuhukimiwa kwa
Masanja Mwinamila kumedhihirisha kwamba matukio mengi ya kuuawa au
kujeruhiwa kwa watu wenye albinism yanapangwa na kufanikishwa na
wanandugu wenyewe kwa sababu ya mawazo potofu ya kutafuta utajiri kwa
njia za mkato.
Kama alivyoeleza Kaimu Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Tabora, ACP. Juma Bwire, Juni 16, 2015, Masanja alithubutu
kwenda kumnyakua mtoto huyo Margret Hamisi (6) majira ya saa 3 usiku na
kukimbia naye gizani akiwa na lengo la kumuuza ajipatie utajiri.
Lakini habari kutoka eneo la tukio
zinaeleza kwamba, haikuwa kazi rahisi kwa wanausalama kumwokoa binti
huyo akiwa hai na kumtia mbaroni mtuhumiwa, kwani walilazimika kujifanya
‘wanunuzi’ ili kuweka mtego wa kumkamata mtuhumiwa na kumwokoa mateka.
Taarifa za uchunguzi zinaeleza kwamba,
mtuhumiwa huyo alianza mchakato wa kutafuta ‘soko’ la kumuuza mtoto wa
dada yake mapema mwezi Juni 2015, lakini wasamaria wema wakawaarifu
wanausalama kuhusu kinachotaka kutokea katika eneo hilo.
Ilibidi maofisa wawili wa usalama
wapangiwe kazi ambapo mmoja alijifanya mnunuzi na mwingine mganga wa
jadi anayeambatana na ‘tajiri’ huyo feki ambao walikutanishwa na
mtuhumiwa huyo aliyewaeleza kwamba ‘dili la albino lipo’.
“Alisema kuna dada yake mwenye albinism
ambaye ana watoto wawili – wa kiume na wa kike – ambaonao wana albinism,
huyo dada ni mtoto wa baba yake mdogo ambaye alifariki mwaka jana
(2014), hivyo nyumbani hakuna mtu wa kiume wa kuleta upinzani.
“Akasema kwamba biashara hiyo ingefanyika
sana, kwani alipanga kuanza kumuuza mtoto wa kike, halafu angemuuza
yule wa kiume na hatimaye kummalizia dada yake!” kilisema chanzo cha
ndani kutoka eneo la tukio.
Kwa kawaida asilimia kubwa ya wakazi wa
Kanda ya Ziwa ni wapagani na wanawaamini waganga wa jadi kuliko mtu
yeyote, hiyo alipokutanishwa na watu hao wawili, mtuhumiwa Masanja
Mwinamila aliamini kila alichoambiwa na ‘mganga’.
Mganga huyo feki, mbali ya kumpigia ramli
na kumwogesha dawa kwenye njiapanda, alimtaka mtuhumiwa kuleta mtoto
huyo akiwa hai kwa maelezo kwamba inabidi ‘afanye tambiko ili dawa
zifanye kazi’, lakini lengo likiwa kumzuia mtuhumiwa asimdhuru mtoto na
hivyo kupata nafasi ya kumwokoa.
Akiwa na shauku kubwa ya kupata mamilioni
ya fedha, baada ya kukubali masharti ya mganga, Masanja alimuomba
‘tajiri’ atafute bunduki ili wakati yeye atakapomnyakua mtoto, wafyatue
risasi hewani kuwatisha watu watakaokimbilia eneo la tukio mara yowe
litakapopigwa.
Taarifa zinasema, wanausalama waliposikia
kauli hiyo wakahisi mtuhumiwa angeweza kwenda hata na panga na
kuwajeruhi watu atakaowakuta eneo la tukio ili amchukue mtoto, hivyo
mganga huyo akatoa masharti kwamba hata kama bunduki itapatikana, lakini
asingependa kuona damu inamwagika kwa yeyote huku akimwaminisha kwamba
dawa atakazoogeshwa zitamfanya awe ‘kiza’ asionekane na mtu yeyote.
Takriban mara tatu zoezi hilo
liliahirishwa kwa kuangalia mazingira ya kiusalama, lakini baada ya
wanausalama kujipanga vyema, ndipo Juni 15, 2015 wakafanikisha mtego huo
na kumkamata mtuhumiwa akiwa amembeba mtoto ambaye alinyakuliwa akiwa
usingizini.
“Ilikuwa ni kazi ngumu, lakini kama siyo
imani kwa mganga, ingekuwa hatari sana hata kwa wanausalama wenyewe.
Jamaa alipewa masharti kwamba, mtoto huyo anayeuzwa anatakiwa afikishwe
kwa mganga akiwa hai bila kujeruhiwa mahali popote; Familia
itakayovamiwa pia isimwage damu; Fedha za manunuzi kabla ya kukabidhiwa
mlengwa lazima zifanyiwe tambiko na masharti ya matumizi; hakutakiwa
kufanya zianaa siku nne kabla ya tukio; na lazima kuogeshwa dawa wale
wote watakaokwenda kwenye tukio,” kilifafanua chanzo kingine.
Bi. Joyce Mwandu Nkimbui (33), ambaye ni
mama wa Margret, anasema siku tatu mfululizo kabla ya tukio, mtuhumiwa
huyo ambaye ni kaka yake anayeishi jirani na hapo alikuwa akija asubuhi
na jioni akijifanya kuja kusalimia na wakati mwingine hata kupikiwa
chakula.
Hata hivyo, alishangaa kukuta kwamba
ndiye aliyevamia nyumbani kwao usiku wa Juni 15, 2015 na kumwamuru
asikimbie kabla yeye hajaingia ndani na kumkwapua mtoto.
“Walikuja usiku, sijui walikuwa wangapi,
lakini wakanilazimisha ‘wewe mama tulia’, nikaogopa na kukimbilia kwenye
majani, nikaanguka kwa sababu sioni vizuri usiku, nikakutana na
mwenyekiti wa kitongoji, ambaye tulikwenda naye nyumbani na kukuta
tayari mtoto hayupo,” Joyce alisema kwa masikitiko.
Matukio mbalimbali.
Tangu mwaka 2006 serikali imekuwa
ikipambana na matukio ya kuuawa na kujeruhiwa kwa watu wenye albinism
nchini, ambapo tayari watu zaidi ya 10 wamehukumiwa kunyongwa, wengine
kesi zao ziko mahakamani na watuhumiwa wengine wanaendelea kusakwa kwa
kuhusika na matukio hayo ya kutisha.
Wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku
ya wenye albinism duniani jijini Arusha Juni 13, 2015, Rais Jakaya
Kikwete alisisitiza kuwa kati ya watu 13 waliohukumiwa kunyongwa wawili
kesi zao zipo katika hatua ya mwisho kufikishwa kwake na kuahidi
zitakapofika mezani kwake atazitendea haki stahiki.
"Lakini mwaka 2014 hadi 2015 serikali
tumepambana na watu wakatili dhidi ya walemavu kwa kuwakamata watu
25 kati yao sita kesi zao zipo mahakamani, huku watano upelelezi
unaendelea na 11 wameachiwa huru kwa kutopatikana na hatia," alisema.
Rais Kikwete pia aliwahakikishia wenye
albinism kupatiwa vifaa vya kupambana na kansa ya ngozi bure kwenye
hospitali za serikali.
Mwaka 2009, Waziri Mkuu Mizengo Pinda
aliangua kilio bungeni kuonyesha uchungu alionao dhidi ya vitendo vya
mauaji ya kikatili ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), na machozi
yake yakayeyusha hoja ya wabunge wa upinzani waliokuwa wamepania
kumbana, ili ajiuzulu kwa madai kwamba, alitoa amri ya kuua wauaji
ambayo ni kinyume na katiba ya nchi.
0 comments:
Post a Comment