ZAIDI ya wanawake 4,000 hufariki dunia
kila mwaka nchini kutokana na kuugua saratani ya shingo ya kizazi huku
wanawake 6241 wakipata ugonjwa huo kila mwaka, wakati wenye umri wa
kuanzia miaka 15 wakiwa kwenye hatari ya kuugua ugunjwa huo.
Dr. Fadhili Emily wa The Fadhaget Sanitarium Clinic Tanzania
Utafiti umebaini kuwa wanawake 10.8 milioni nchini wako kwenye hatari ya kuugua ugonjwa huo.
Virusi vinavyoweza kusababisha saratani hiyo viko vya aina 13, lakini chanjo hiyo imelenga virusi vya aina mbili ambavyo vinachangia asilimia 70 ya saratani zote.
Wanawake ni walinzi wakubwa katika familia na wamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa familia zinafuata maadili mema.
Mbali ya kuwa na jukumu hilo pia wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa familia zinaishi katika mazingira bora na kuwa na maendeleo.
Pamoja na kuwepo kwa juhudi hizo bado kumekuwa na idadi kubwa ya wanawake wanaokufa kutokana na magonjwa mbalimbali.
Kuna magonjwa mengi yanayowasumbua wanawake na kusababisha kupoteza maisha huku wengine wakishindwa kupata huduma bora.
Saratani ya shingo ya kizazi ni kati ya magonjwa yanayosababisha wanawake wengi kupoteza maisha kutokana na kutofahamu uwepo wa tatizo hilo.
Kwa mujibu wa jarida la 'ni tatizo langu' linatuhusu sote' inaeleza kuwa saratani ya shingo ya kizazi inashika nafasi ya pili baina ya saratani za wanawake duniani kote.
Kijarida hicho kinaeleza kuwa, zaidi ya wanawake laki tano hupata maambukizi ya saratani ya shingo ya kizazi kila mwaka ambapo zaidi ya asilimia 80 ya wanawake wanaishi kwenye nchi maskini.
Pia inaeleza kuwa, zaidi ya vifo 274,000 vya wanawake vinasababishwa na ugonjwa huo kila mwaka ambapo kila baada ya dakika mbili, mwanamke mmoja hufariki kutokana na saratani ya shingo ya kizazi duniani kote.
Katika kila wanawake wawili wanaofariki kwa saratani, mmoja hufariki kwa saratani ya shingo ya kizazi ambapo hushika nafasi ya pili katika saratani za wanawake na ndio sababu kubwa ya vifo vya wanawake katika nchi zinazoendelea.
"Takwimu zilizotajwa hapo juu sio namba tu, zinawakilisha wake zetu, mama zetu, mabinti zetu na rafiki zetu, mara nyingi kwenye umri tunapowahitaji sana hupoteza maisha," ilieleza.
Dalili za mwanzo wa saratani ya kizazi hutokea wakati chembe za sehemu yoyote ya mwili zinapokuwa bila mpangilio maalumu na ukuaji usio na mpangilio wa chembe hai katika shingo ya kizazi ' shingo ya ya kizazi ni sehemu ya mfuko wa uzazi inayounganisha sehemu ya ndani na nje'.
Saratani ya shingo ya kizazi ni tatizo hatari linaloweza kusababisha kifo ambalo husababishwa na virusi viitwavyo 'Human Papilloma Virus' (HPV) iwapo kinga ya mwili ikishindwa kuondoa hayo maambukizi, chembe hai za kawaida huanza kukua bila mpangilio na kusababisha dalili za awali za saratani.
Inaelezwa kuwa iwapo maambukizi hayo yataendelea kwa muda mrefu ukuaji wa saratani ya shingo ya kizazi huanza kutokea ambapo kunaweza kuchukua miaka 10-20 tangu kuambukizwa au miaka miwili tu kutokea kwa saratani.
Kuna aina za HPV 100, kati ya hizo 15 husababisha saratani ya shingo ya kizazi wakati HPV aina 16 na 18 kwa pamoja husababisha asilimia 70 ya saratani zote za shingo ya kizazi na hizi aina mbili za virusi ndio zinatambulika sasa kusababisha saratani hii ambapo asilimi 99.7 ya saratani ya shingo ya kizazi inahusishwa na maambukizi ya HPV.
Kirusi cha HPV huenezwa kwa njia ya kugusana sehemu za siri, hivyo maambukizi yanaweza kutokea hata kama tendo la kujamiiana halijahusisha muingiliano wa sehemu za siri ambapo mpira wa kiume unaweza kupunguza maambukizi lakini si kwa asilimia 100.
Maambukizi ni makubwa kwa wanawake wenye umri chini ya miaka 25 ambapo wanawake waliokwishaambukizwa na HPV na miili yao haijapambana na kuondoa virusi, vinaweza kupata saratani na dalili za mwanzo za saratani ambapo maambukizi mengi ya HPV huondolewa na kuuliwa na kinga ya mwili wa binadamu.
Kuna baadhi ya vitu vinavyochangia maambukizi ya HPV ni kuanza kufanye tendo la kujamiiana katika umri mdogo, upungufu wa kinga mwilini, kurithishana kati ya vizazi, maambukizi ya HPV 16 na 18 ambayo hupelekea kugawanyika kwa chembe hai bila mpangilio, ugonjwa mkanda wa jeshi, kuzaa watoto wengi, upungufu wa madini ya folic acid na magonjwa ya ngono yanayojirudia.
Hakuna dalili zinazojitokeza katika hatua za mwanzo za maambukizi lakini katika hatua za mbele za ugonjwa kuna dalili zinazojitokeza kama kutokwa na damu ukeni kusiko kwa kawaida kwa uzito au wakati unaokuja, maumivu makali wakati wa tendo la kujamiiana, kuvimba kwenye kinena na kutokwa haja ndogo na kubwa kusikozuilika.
Hata hivyo dalili hizo zinaweza kutokea kwenye magonjwa mengine zaidi ya saratani ya shingo ya kizazi ni vizuri kupata ushauri wa daktari ili ajue tatizo linalosababisha dalili hizo.
Endapo upimaji utafanyika kwa ufasaha utapeleka ugunduzi mapema na matibabu ya dalili za mwanzo za saratani hupelekea kuzuia kuendelea kwa ugonjwa na hatimaye hupunguza hatari ya vifo vitokanavyo na saratani ya shingo.
Uchunguzi sahihi wa kujua hatua ya saratani ilipofikia ni muhimu ili kujua njia sahihi ya matibabu ambapo njia za matibabu ni Hysterectomy hii ni kuondoa kwa kizazi chote pamoja na shingo ya kizazi pia mirija ya kupitisha mayai yanaweza kutolewa.
Njia nyingine za matibabu ni Trachelectomy njia hii ya shingo hutolewa na kubakisha mfuko wa uzazi kwa ajili ya uzazi hapo siku za baadaye njia nyingine ni Radiotherapy hii ni njia ya mionzi hutumika kutibu saratani iliyosambaa na njia nyingine ni Chemotherapy hii ni njia ya dawa za vidonge na sindano ili kutibu saratani.
Saratani ya shingo ya kizazi na matibabu yake yanaweza kusababisha mabadiliko makubwa katika hali ya maisha kipindi chote cha matibabu na hata miaka mingi baada ya matibabu.
Vilevile uchunguzi na matibabu ya dalili za mwanzo za saratani ya shingo ya kizazi yanaweza kuleta hali ya wasiwasi.
Chanjo zimegundulika hivi karibuni na sasa zinatumika duniani kote ambapo matumizi ya chanjo yatasaidia sana kupunguza ukubwa wa tatizo hilo.
Ni muhimu kufanya chanjo na uchunguzi kama njia zinazoshabihiana katika kuzuia saratani ya shingo ya kizazi ili kujikinga kwa asilimia kubwa na saratani hii.
Chanjo pamoja na uchunguzi vitasaidia kupunguza hatari ya ugonjwa huu zaidi ya kufanya uchunguzi peke yake na pia vitasaidia kupunguza idadi ya matokeo ya uchunguzi yaliyo na shida na yanayohitajika kutatuliwa.
Chanjo hiyo ina uwezo wa kudumu kwa miaka 15 hadi 20 na kwamba zaidi ya nchi 100 duniani tayari zimeanza kuitumia chanjo hiyo.
0 comments:
Post a Comment