Ni nini tatizo la kupata haja kubwa?
Ni haja kubwa inayopatikana isiyozidi mara tatu katika wiki na ama
haja kubwa inayoleta shida kutoka kwake na utokaji wake ni mithili ya
mavi ya mbuzi (uyabisi) hata kama inapatikana kila siku. Hali hii
inaposhamiri muathirika hupata choo si zaidi ya mara tatu katika kipindi
cha mwezi mmoja.
Ni moja miongoni mwa matatizo katika mfumo wa kusaga chakula
yanayowakumba watu wengi si hapa kwetu Zanzibar tu bali dunia nzima kwa
jumla. Shida ya kupata choo ni hali inayowakabili watu mbalimbali.
Dr. Fadhili Emily
Dr. Fadhili Emily
Takriban ni wastan wa asilimia kumi na mbili ya watu duniani
wanasadikiwa kuwa na tatizo la kuchelewa kupata haja kubwa. Katika hali
ya kawaida mwanadamu hupata haja kubwa karibu kila siku au kila baada ya
siku moja.
Kwa mtoto mchanga baada kuzaliwa huenda haja mara nne hadi tano kwa
siku. Wale wanaonyonya maziwa ya mama (maziwa ya kifua) hupata haja mara
nyingi zaidi ukilinganisha na wenzao wanaonyonya maziwa ya kopo yaani
fomula (formula). Kwani baadhi yao hupata haja kila baada ya kunyonya
wakati wenzao wa maziwa ya kopo hupata haja mara moja tu kwa kila baada
siku mbili hadi tatu. Mtoto anaenyonya maziwa ya mama si aghlabu kupata
shida ya haja kubwa. Anapotimiza umri wa miaka miwili mtoto hupata choo
takriban mara moja hadi mbili kwa siku. Wakati mtoto wa umri wa miaka
minne anapata haja kubwa mara moja kwa siku.
Jee hali ikoje hapa kwetu Zanzibar?
Katika kliniki zetu za upasuaji karibu asilimia kubwa ya wagonjwa
wanaokuja kwa tatizo la kuumwa na tumbo wengi wao hubainika kuwa na hali
isiyoridhisha katika masuala ya kupata haja kubwa. Aidha wagonjwa hao
wamekuwa wakilalamika kuchelewa kupata au hupata haja kubwa kwa shida
kabisa. Kwa watoto wachanga hali hii pia ipo, na kwa watu wazima kina
mama husumbuliwa zaidi ukilinganisha na kina baba. Wazee nao hasa
kwasababu ya umri ambapo maradhi mengi hujitokeza na pia kutoweza
kujituma kama ilivyo kwa vijana, husumbuliwa na tatizo hili kwa kiasi
kikubwa. Watu wengi wamekuwa wakijitibu wenyewe pasipo kujua nini hasa
kinawasibu. Hali hiyo hupelekea kwa baadhi yao kupata madhara zaidi
wasiyoyatarajia. Mathalan hupata vidonda vya tumbo, maumivu ya tumbo
yasiokwisha, kuharisha mara kwa mara, na baadhi yao chango huziba hali
inayowapelekea kufanyiwa opresheni ya dharura.
Kuchelewa kupata haja kubwa huwa ni sababu kuu ya kupata maumivu
wakati wa kwenda haja. Hali inapokuwa mbaya mtu hukosa kabisa kupata
choo na kujamba pia, na uchango wake mkubwa hujaa kinyesi. Kushindwa
kupata haja kubwa ni dalili inayotokana na sababu nyingi. Sababu zenyewe
zimejigawa namna mbili. Mosi, kuziba choo, na pili ni uchango kuwa na
mwendo wa taratibu mno.
SABABU
Zipo sababu kadhaa zinazopelekea kutokea kwa tatizo la kukosa kupata
haja kubwa kikawaida, miongoni mwa hizo ni kama hizi zifuatazo:
- Inaweza ikawa yenyewe tu bila kusababishwa na hali yoyote ile kama vile madhara ya dawa
fulani, au hali ya kiafya, na huwa haiambatani na maumivu ya tumbo.
Kwa lugha nyengine ni kwamba sababu hasa huwa haijulikani. Hii ndio
sababu maarufu kuliko nyengine zote.
- Inaweza kusababishwa na mpangilio mbaya wa chakula, kutokula vyakula vyenye fiber (nyuzinyuzi), kunywa maji kidogo kuliko inavyotakiwa.
- Matumizi ya dawa mbalimbali na baadhi ya athari zake kama vile baadhi ya dawa za kutibu presha (shinikizo la damu), dawa za kupunguza maumivu, dawa za kutibu degedege, dawa za kutibu mamivu ya tumbo ikiwa pamoja na dawa za kutibu mfadhaiko, dawa za kutibu alaji (makole).
- Mgonjwa wa maradhi ya kisukari, maradhi ya misuli.
- Maradhi ya uvimbe katika uti wa mgongo, kansa ya utumbo mkubwa, kidonda/kuchanika njia ya haja kubwa mlangoni yaani fisha (anal fissure).
- Kwa makusudi tu mtu hujizuwia asiende haja kwa sababu labda hakuna choo cha kuridhisha, anaogopa maumivu hasa wale wenye fisha (anal fissure), ama kwa uvivu tu.
- Watoto nao hupata tatizo la kuzaliwa nalo. Kukosekana mishipa ya fahamu katika sehemu ya utumbo mkubwa huwa ndio sababu inayopelekea utumbo huo kutosukuma kinyesi hivyo kusababisha kuchelewa kupata haja kubwa ambapo mara nyengine hupindukia kipindi cha wiki moja hadi mbili au hata zaidi. Kwa maana hiyo tumbo huvimba na mtoto hudhoofu kiafya. Hili ni tatizo la kipekee.
VIPI TUNACHUNGUZA
Maelezo ama dalili mgonjwa anazozielezea jinsi anavyosumbuka kupata
haja kubwa, pekee hutoa taswira kamili ya tatizo linalomkabili. Miongoni
mwa dalili hizo ni zile pamoja na kuwa na choo kigumu, hutoka kwa
shida, hufanana na mavi ya mbuzi ama sungura yaani uyabisi. Dalili
nyengine ni mbweo, kuvimba tumbo, maumivu ya tumbo, kuumwa na kichwa,
uchovu, kutojiskia vizuri na pia kuwa na hisia za kutomaliza haja yote.
Na anapoulizwa mgonjwa juu ya mpangilio wake wa mlo mara nyingi
hubainika kutokutumia vyakula vyenye nyuzinyuzi (hivi ni vyakula vya
sehemu ya mimea ambayo haisagwi na mwili wetu na hivyo kusukuma utumbo,
huku ikifyonza maji wakati ikitoka na kufanikisha kupata haja kubwa).
Wengi wao hawali nafaka, mboga za majani, na matunda kama mlo wa
kawaida. Kutokunywa maji ya kutosha, kutofanya mazoezi kikawaida au
wakati mwengine husababishwa na matumizi ya baadhi ya dawa ambazo kwa
kuzitumia kwa kipindi cha muda mrefu hatimae huleta athari ya kuzuwia au
kuchelewa kupata choo.
Tunachunguza kwa kuliangalia na kugusa tumbo, ikibidi huangalia njia
ya haja kubwa, wakati mwengine hata kwa kutumia darubini maalum tunaweza
kubaini tatizo hilo. Xray ya tumbo ingawa si lazima, nayo pia huweza kutumika kubainisha uwepo wa tatizo.
KINGA
JE, VIPI TUNAWEZA KUJIKINGA?
Ni rahisi zaidi kukinga usipate hali hii kuliko kutibu. Mara au pindi
ukipata nafuu jambo la msingi ni kujitahidi kuendeleza mazoezi kwa
maana ya matembezi, kuogelea, au kushiriki michezo ya aina yoyote ile
ilimradi tu utoke jasho. Kunywa maji kiasi cha kutosha ambacho kwa
wastani mtu mzima anatakiwa kwa siku anywe lita mbili hadi mbili na nusu
kulingana na hali ya hewa. Kula mboga za majani kama vile mchicha,
kisambu, mtoriro, kabichi, karoti na nyenginezo; nafaka kwa mfano
karanga, mahindi, ngano, fiwi, mbaazi, kunde, maharage, njugu mawe na
kadhalika; pendelea kula matunda hususan ndizi mbivu, embe, chenza na
machungwa (kula hadi maganda ya ndani), papai, balungi, pea(parachichi),
fenesi, epul (usilimenye), shelisheli na mengine mengi tu ambayo kwa
kweli katika mazingira yetu Mola ametujaalia tunayo mengi sihaba. Yote
haya hutengeneza mazingira mazuri ya kupata haja kubwa kikawaida na bila
shida yoyote.
Na kwa watoto ni kuwapangia muda wa kwenda kujisaidia mapema asubuhi na kipindi cha takriban dakika thelathini baada kupata mlo.
NINI HASA KAZI YA VYAKULA VYENYE NYUZINYUZI?
Vyakula vya namna hii kwa kawaida havisagwi na mwili kwahiyo hupita
katika utumbo na kutoka mwilini.Iwapo tutakula nafaka na matunda na
mboga za majani tutakuwa na nafasi kubwa kujikinga kupata maradhi kama
vile, maradhi ya moyo, unene wa maradhi (obesity), kuepuka kupata
bawasili, na hata kusaidia mwili kudhibiti kiwango cha sukari katika
damu kwa kuchelewesha uyeyukaji wake mwilini. Inadhibiti na kupunguza
kiwango cha mafuta mwilini kwa kuambatana nayo. Na kubwa zaidi huwa ni
kinga tosha dhidi ya kansa ya utumbo mkubwa kwani hubeba sumu za kwenye
utumbo na kutoka nazo. Kwa lugha isiyo ya kitaalamu labda tunaweza
kusema na kumithilisha vyakula vya nyuzinyuzi vinafanyakazi kama brashi.
Vinasafisha njia yote ya mfumo wa usagaji chakula.
TIBA
- Ni pamoja na kunywa maji ya kutosha.
- Kula vyakula vyenye nyuzinyuzi (fiber), hivi vingi vinapatikana katika mboga za majani, nafaka na matunda.
- Matumizi ya haluli kama ni tiba inabidi kutumiwa kwa hadhari sana, kwa vile kuzoeleka kwake kunaweza kupelekea uchango ushindwe kufanyakazi wenyewe.
- Nayo upigaji wa bomba hutumiwa zaidi kama kisisimuzi. Hatahivyo bomba huleta manufaa ama matokeo chanya zaidi pale tu kinyesi kinapokuwa kimejikusanya karibu na mlango wa haja kubwa.
ATHARI ZA MATATIZO YA HAJA KUBWA
Kukosa kupata haja kubwa au ama kupata haja kubwa kwa shida ikiwemo
kupata choo kigumu kunaweza kusababisha miongoni mwa maradhi mengine ni
pamoja na kupata bawasili, kidonda ama mpasuko katika mlango wa haja kubwa (fisha), kutoka futuru (mwijiko), mrundikano wa kinyesi
katika uchango. Hali hii ikiachwa kuendelea tumbo litajaa na kuvimba,
litakuwa gumu na lenye maumivu. Mgonjwa anaweza akawa na dalili za kuziba utumbo yaani kutapika na kadhalika.
HADHARI
Siku zote yapaswa tuwe makini na tuchukuwe hadhari pale inapotokezea
kutopata haja kubwa kwa ghafla na ikadumu kwa siku kadhaa. Hali hii
hutokea aghlabu sana kwa wazee na ni moja ya dalili ya kuwepo kwa uvimbe
katika uchango mkubwa ambao mara nyingi huwa ni kansa ya utumbo.
Bilashaka huambatana na dalili nyengine kama vile kutokwa damu njia ya
haja kubwa wakati wa kujisaidia, kuharisha baadhi ya wakati na kupungua
uzito wa mwili au kukonda na kadhalika.
USHAURI
Hapanashaka ili kupunguza tatizo hili ambalo linawakabili watu wengi katika jamii yetu, elimu ya chakula bora na mlo ulopangika ndio jibu sahihi ama muarubaini wa kutilia mkazo. Tuanzie
skuli na majumbani mwetu kuwaelimisha hasa wanetu. Ni kweli kabisa
tumejaaliwa rasilimali nyingi sana kwa maana ya matunda ya msimu
yanayofika kuzagaa kama uchafu na kuharibika, nafaka hadi kuoza ovyo,
mboga za majani za kila aina, lakini la ajabu ni kuona watu wetu wengi
hawajui thamani ya neema hiyo na kutokuitumia kwake ndio chanzo kikubwa
cha maradhi mengi yanayotukabili. Hivyo basi tuwazoweshe watoto wetu
kupenda kula matunda, nafaka na mboga za majani tangu wako wadogo, kwani
si tu hupelekea kupata haja kubwa kikawaida bali pia vyakula hivi
vimejaa vitamini mbalimbali muhimu kwa siha ya mwanadamu.
Muone daktari wako atakuskiliza, atakuchunguza na hatimae atakupa
maelezo yenye tija kwako. Tukumbuke samaki mkunje angali mbichi, udongo
upate ulimaji.
0 comments:
Post a Comment