Tatizo hili pia huitwa ‘Anembryonic gestation’. Hutokea pale mfuko wa mimba unapoendelea kukua bila ya kuwa na kitoto ndani. Kifuko cha mimba huitwa ‘Gestational Sac’ na kitoto ni ‘Embryo’.
Mwanamke anakuwa mjamzito kama kawaida ambapo ana dalili zote za ujauzito na katika wiki sita za mwanzo akifanya Ultrasound kitoto kinaweza kuonekana lakini baada ya hapo unakuta dalili za mimba zinaanza kupungua taratibu na mama akifanya ultrasound mimba itaonekana mfuko wake tu na ndani hakuna kitu. Hapa ndipo tunasema mama amepata Blighted Ovum.
Mimba ilikuwepo sasa imeyeyuka. Hali hii ikiendelea mama ataanza kutokwa na damu ukeni taratibu.
Wakati mwingine mwanamke anaweza kupatwa na tatizo hili hata bila yeye mwenyewe kujijua kama ni mjamzito.
Chanzo cha tatizo
Blighted Ovum ni tatizo linalokatisha tamaa mwanamke anayetafuta ujauzito na wakati mwingine haamini kilichotokea.
Tatizo hili hutokana na hitilafu katika yai lenyewe kutokana na kasoro za Kromozom zinazorutubisha yai, Kromozom zinazorutubisha yai ni za kiume zikiungana na za kike, hivyo mimba ikitungwa na kasoro haiendelei, inatoka mapema.
Mwanamke anaweza kutokewa na tatizo hili hata zaidi ya mara mbili.
Kasoro za Kromozon zinaweza kusababishwa na mambo mengi kama maambukizi, kemikali na mionzi au hali isiyoeleweka. Kromozom za kiume na za kike pia huchangia hali hii.
Kromozom za kike ni aina ya X na zile za kiume ni za aina ya Y. Mwanamke ana aina moja tu ya Kromozom ambazo ni za kike na mwanaume ana Kromozom za aina mbili, za kiume na kike.
Kromozom pia zikichoka husababisha mimba iwe na kasoro hivyo huharibika na kutoka. Kama tulivyoona, mimba inaweza kuyeyuka ghafla na mwanamke anaweza kupoteza hata mimba tatu au zaidi.
Dalili za mimba kuyeyuka
Mwanamke katika hatua za awali anakuwa na dalili zote za ujauzito kama kufunga kupata hedhi ambapo anaweza kufunga hata miezi mitatu, awali anakuwa na dalili nyingine za ujauzito kama kichefuchefu, matiti kujaa na hata kutapika, kipimo cha mkojo ultrasound kuonyesha kwamba ni mjamzito, lakini tatizo linapotokea na dalili za ujauzito huanza kupungua na kupotea kabla hata mimba haijafikisha zaidi ya miezi mitatu.
Kwa hiyo mwanamke anaweza kupotelewa na dalili zote za ujauzito isipokuwa kutokwa na damu ukeni.
Baada ya kupotea dalili za ujauzito kabla damu haijaanza kutoka, ukifanya kipimo cha ultrasound itaonyesha una kifuko cha mimba lakini kimimba hakipo ndani.
Hali hii unaweza ukakaa nayo kwa muda mrefu na mwishowe utaanza kuhisi maumivu ya tumbo chini ya kitovu, maumivu ya kiuno, kukaza kiuno na kuhisi kama unataka kupata damu.
Uchunguzi
Tatizo hili katika hatua za awali mwanamke hupima mkojo wa mimba pale anapohisi dalili za ujauzito zinaanza kupotea hivyo kipimo kitaonyesha kufifia kwa ule mstari mwekundu unaothibitisha ujauzito.
Baada ya hapo afanye ultrasound ndipo itaonyesha kuyeyuka kwa mimba.
Kufifia kwa dalili za ujauzito inaashiria kutoweka au kupungua homoni muhimu zinazotoka mara tu mimba inapokuwa hai.
Baada ya muda kama ni zaidi ya miezi mitatu mwanamke ataanza kutokwa na damu ukeni taratibu kuashiria mimba inatishia kutoka na baadaye damu itatoka nyingi na nzito na maumivu makali sana.
Mimba hiyo isiyo rasmi inaweza kutoka yote au isitoke yote.
Hali hii ya kuyeyuka kwa mimba inapotokea ni vema mwanamke akafanyiwe uchunguzi wa kina ikibidi hata mwanaume naye afanyiwe uchunguzi vinginevyo kila mimba atakayopata itaishia kupotea.
Nini cha kufanya?
Endapo mwanamke atakuwa na tatizo hili na likajirudia, yaani kila ukipata mimba haizidi miezi mitatu inapotea, amuone daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama na uzazi katika hospitali za mikoa na wilaya kwa uchunguzi wa kina.
0 comments:
Post a Comment