Wasiliana Nasi

Wasiliana Nasi

Tuesday, January 13, 2015

MUUMINI WA KANISA LA JEHOVA WITNESS BWANA RICHARD ABDON JUMA AKATAA KUONGEZEWA DAMU


 Muumini wa Kanisa la Jehova Witness, Richard Abdoni Juma, 44, (pichani), mkazi wa Mtaa wa Migera wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, ambaye alitarajiwa kufanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kutokana na ajali, madaktari wameshindwa kufanya hivyo kutokana na imani ya dini yao.
Bw. Richard Abdoni Juma, (44) anayedaiwa kupata ajali na kuvunjika nyonga.

AGUNDULIKA HANA DAMU
Akizungumza na waandishi wa gazeti hili wiki iliyopita katika wodi namba 17, Sewahaji mgonjwa huyo alisema kwamba madaktari waligundua kuwa amepungukiwa damu hivyo walimuomba aongezewe kwanza ndipo wamfanyie upasuaji lakini alikataa.
“Nimekataa kuongezewa damu kutokana na imani ya dini yangu ya Jehova Witness ambayo inakataza mtu kuongezewa damu.
“Baada ya kuwaambia madaktari hao hilo walinishauri nitumie vyakula vinavyoongeza damu yakiwemo matunda na wakasema watanifanyia upasuaji baada ya damu kuongezeka.

CHANZO CHA TATIZO
“Nakumbuka ilikuwa Jumapili ya Desemba 28, mwaka jana saa 7 mchana maeneo ya Amgembe Nyangoye wakati nikitoka kanisani kusali huku nikiwa nimempakia mwanangu Lucas (11) kwenye pikipiki ndipo gari dogo ghafla lilikatisha barabara tukaligonga wote tukaanguka na kuumia.
“Mwanangu Lucas aliumia vidole na mguu, mimi nilihisi maumivu makali sana mwili mzima lakini nyonga ndiyo ilikuwa ikiniuma zaidi, wasamaria wema walifika na kutuchukua kisha kutukimbiza katika Hospitali ya Wilaya Bukoba.
“Hali ilizidi kuwa mbaya kitendo kilichofanya madaktari wanihamishie katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza baada ya wiki moja kupita, wakati huo mwanangu alibaki hospitali ya Bukoba kisha akaruhusiwa kwenda nyumbani.

NILIGUNDULIKA NYONGA IMEVUNJIKA
“Nikiwa katika Hospitali ya Bugando nilifanyiwa uchunguzi sambamba na vipimo ikagundulika kuwa nyonga imevunjika hivyo nihamishiwe katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
“Nilipewa matumaini kwamba katika hospitali hiyo kuna madaktari bingwa na ilipofika Jumanne ya wiki hii (wiki iliyopita) nikahamishiwa hapa.
Richard Abdoni Juma akiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

MADAKTARI WATAKA KUMPASUA
“Mbali na kugundulika kuwa nyonga ilivunjika lakini ilibainika kuwa nina upungufu wa damu hivyo natakiwa kuongezewa damu kwanza ndipo nifanyiwe upasuaji, hata hivyo, kutokana na imani ya dini yetu nilikataa.
“Imani yetu haturuhusiwi kuongezewa damu hivyo madaktari nilipowaambia hivyo wakaahirisha zoezi hilo.
“Badala yake walinishauri nitumie matunda mbalimbali kwa imani kuwa ndani ya wiki moja damu itakuwa imeongezeka ndipo watakaponifanyia upasuaji.

NATUMIA MATUNDA YA KUONGEZA DAMU
“Kutokana na ushauri huo sasa natumia matunda ya kuongeza damu kwa wingi hivyo naamini baada ya muda huo walionishauri nitakuwa nimeimarika.

KAZI YAKE
“Mimi ni fundi ujenzi na nina mke na watoto watatu ambao wananitegemea lakini kwa sasa wamekosa matumaini ya kuishi kutokana na kuwepo kwangu kitandani, sijiwezi, kuinuka nimekuwa ni mtu wa kujisaidia hapahapa nilipo, ni mtu wa kuogeshwa.
“Ninawashukuru madaktari na manesi wa hapa Muhimbili kwa kunipa huduma za karibu, nawaombeni Watanzania mnisaidie kwa kupitia namba yangu 0784 969568 au 0763 196457,” alisema Richard akiwa amejilaza kitandani.

0 comments:

Post a Comment