UNFPA, UNICEF, Shirikisho la Kimataifa la Wakunga na Shirikisho la Kimataifa la Magonjwa ya Wanawake na Uzazi.Wito kwa wafanyakazi wa afya duniani kote ili kuhamasisha kukomesha ukeketaji
Kwa mwaka 2015, ujumbe wa kimataifa wa siku ya kupinga ukeketaji umewalenga wahudumu wa afya; “Uhamasishaji na ushirikishwaji wa wafanyakazi wa Afya ili kuharakisha kutokomeza ukeketaji”. Na hii ni kwa sababu asilimia 34 ya ukeketaji duniani hufanywa na wahudumu wa afya.Pamoja na ujumbe huu mahsusi kwa wahudumu wa afya, wadau wengine wote unawahusu.
Ujumbe unasema hivi:
Ukeketaji wa wasichana na wanawake unakiuka haki za binadamu na unadhoofisha afya na ustawi wa wasichana takriban milioni 3 kila mwaka. Zaidi ya wasichana na wanawake milioni 130 katika nchi 29 barani Afrika na Mashariki ya Kati ambapo hadi leo hii vitendo hivi vimekithiri wamekwisha fanyiwa aina fulani ya ukeketaji - na athari kwa maisha yao ni kubwa sana.
Duniani kote, tunashuhudia kuongezeka kwa utayari wa jamii na serikali ili kuondokana na vitendo vya ukeketaji - lakini hii haitoshi kwani jitihada zaidi zinahitajika. Leo, tunapoadhimisha Siku ya Kimataifa ya kukomesha ukeketaji dhidi ya watoto wa kike, tunatoa wito kwa wafanyakazi wote wa afya – kuanzia wakunga, wauguzi madaktari wa magonjwa ya wanawake na watu wote katika sekta ya Afya kutoa hamasa dhidi ya kukomesha vitendo vya ukeketaji wa watoto wa kike.
Mchango wa wafanyakazi wa sekta afya katika jitihada za kimataifa za kukomesha ukeketaji dhidi ya watoto wa kike ni muhimu sana kwani wana uelewa mpana wa mienendo na desturi ya kijamii katika jumuiya wanazozihudumia. Hivyo wafanyakazi wa afya wanaweza kuharakisha kupungua kwa kasi kwa vitendo vya ukeketaji kwani watu wanaowahudumia wana imani kubwa dhidi yao.
Wafanyakazi wa afya pia wana uelewa wa kina juu ya madhara yanayotokana na vitendo vya ukeketaji kwani wanashuhudia madhara katika njia ya mkojo, njia ya hedhi, maambukizi katika via vya uzazi ikiwa ni pamoja na kutoka damu nyingi na hatimae vifo, pia hushuhudia athari za kisaikolojia dhidi ya wale waliofanyiwa vitendo vya ukeketaji hali ambayo ni ya kudumu katika maisha yao.
Wafanyakazi wa afya pia wapo katika nafasi nzuri ya kuongoza jitihada za kupinga mienendo mibaya inayoibuka katika nchi nyingi.Katika baadhi nchi ukeketaji unafanywa na wahudumu wa afya, mathalan takriban msichana mmoja kati ya watano wamekeketwa na watoa huduma waliopatiwa mafunzo, na katika nchi zingine idadi hii inaongezeka inafikia kati ya wasichana watatu hadi wanne.
Ukeketaji ni kinyume cha sheria katika nchi nyingi, Tanzania ikiwemo chini ya sheria ya masuala ya kujamiiana 1998, na watoa huduma za afya ambao wanafanya vitendo hivyo katika maeneo haya wana vunja sheria. Ifahamike kuwa katika nchi zote, aidha sheria zao ziwe zinaruhusu au haziruhusu vitendo vya ukeketaji ni kukiuka haki za msingi za wanawake na wasichana.
Wataalamu wa afya hususan wale walio katika zahanati na vituo vya afya mara nyingi wanaweza kuwa na shinikizo kubwa la kufanya ukeketaji. Lakini endapo watahamasishwa kupinga shinikizo hilo, wanaweza kuwa sehemu ya ufumbuzi.
Hivyo, kwanza kabisa, tunatoa wito kwa wafanyakazi wote wa afya kama wapo wanaoshiriki vitendo vya ukeketaji kuachana na vitendo hivyo na kutumia ushawishi walionao katika jamii wanazofanyia kazi na kuhamasisha wenzao katika jamii zingine kukomesha vitendo vya ukeketaji katika maeneo yote. Pia tunatoa wito kwa wafanyakazi wote wa afya kulinda afya ya uzazi na ujinsia ya wasichana wote ambao tayari wamekeketwa.
Tunajua kwamba wafanyakazi wa afya hawawezi kufanya hivyo peke yao. Mashirika kama UNFPA, na UNICEF, kupitia mpango wetu wa Pamoja wa kukomesha ukeketaji, pamoja na Shirikisho la kimataifa la Wakunga, na Shirikisho la Kimataifa la magonjwa ya wanawake na uzazi, tuko tayari na tunayo nia ya kusaidia jitihada za kuwapatia wafanyakazi wa afya ujuzi na taarifa yoyote itakayohitajika ili kuongeza kasi katika kukomesha ukeketaji na pia kutoa tiba dhidi ya madhara yaliyotokana na ukeketaji.
Kanuni za kijamii, hususan katika jamii ambazo zina mshikamano na umoja huwa zina nguvu kubwa juu ya maisha na mienendo ya jamii husika. Lakini kanuni hizi zinaweza kubadilika endapo watu wataamua kufanya hivyo. Pia endapo wafanyakazi wa afya, viongozi, wataalam, na, zaidi ya yote, wasichana na familia kwa ujumla, watakemea na kuchukua hatua dhidi ya mienendo mibaya.
Katika Siku ya Kimataifa ya kukomesha ukeketaji, Tushikamane kupinga ukeketaji kwani Afya, Haki na Ustawi wa mamilioni ya wasichana unategemea umoja wetu.
0 comments:
Post a Comment