Mshituko wa moyo unatokea wakati mtiririko wa damu yenye oksijeni unapozuiwa kwa ghafla katika misuli ya moyo. Iwapo mzunguko huo wa damu hautaendelea haraka, kitendo hicho huifanya misuli ya moyo kuharibika kwa kukosa oksijeni na hivyo kuhatarisha maisha ya muathirika.
Mshituko wa moyo kwa lugha ya tiba unajulikana kama ‘Myocardial Infarction’ inayomaanisha “Myo” muscles au msuli, ‘cardio’.... Heart au moyo na “infarct”....kufa kwa tishu kutokana na kukosa oksijeni.
Kama vilivyo viungo vingine mwilini hasa misuli, moyo nao huhitajia damu.
Bila damu seli za moyo hudhoofika suala linalosababisha mtu kuhisi maumivu. Mshituko wa moyo au Heart Attack kama hutaki kutumia myocardial onfarction, hutokea pale mshipa mmoja wa damu au zaidi inaposhindwa kusafirisha damu yenye oksijeni katika moyo, kutokana na kuziba mishipa hiyo.
Mishipa ya damu inaweza kuziba kwa sababu tofauti kama vile, kuta za mishipa ya damu inayopeleka damu kwenye moyo (coronary arteries) kuwa nene, chembechembe za mafuta kujikusanya katika mishipa ya damu, kudhoofika na kukonda mishipa ya damu, mishipa ya damu inaposinyaa na kushikana au spasm na kujitokeza donge la damu katika mishipa ya damu.
Mshituko wa moyo mara nyingi husababishwa na ugonjwa wa moyo wa mishipa ya damu au Coronary Heart Disease (CHD). Hii ni hali ambayo ndani ya mishipa ya damu hutokea kitu kiitwacho ‘plaque’ na kuzuia damu isiweze kupita katika mishipa ya damu, ambayo ni matokeo ya muda mrefu. Lakini ni wakati gani mtu hukabiliwa na hatari ya kupata mshituko wa moyo?
Ni pale umri wa mtu unapoongezeka na kuwa mzee, mtu anapokuwa na unene wa kupindukia, kuvuta sigara, kuwa na shinikizo la damu au High Blood Pressure. Kuishi bila kuwa na harakati na kutoushughulisha mwili.
Mtu kuwa na kiwango cha juu cha mafuta katika damu au High Blood Cholesterol. Kuwa na ugonjwa wa kisukari na kuwa na msongo wa mawazo, wasiwasi na fikra nyingi. Mambo mengine yanayochangia kupata mshituko wa moyo ni baadhi ya magonjwa ya moyo, kufanyiwa upasuaji wa moyo, kuwa na ndugu katika familia ambao wana matatizo ya moyo na jinsia ya kiume.
Uvutaji sigara husababisha mshituko wa moyo unaotokana na kuziba mishipa ya damu kwa asilimia 36, ambapo unene husababisha ugonjwa huo kwa asilimia 20. Kukaa bila kujishughulisha au kufanya mazoezi husababisha mshituko wa moyo kwa asilimia 7-12. Pia wanaume wanakabiliwa na hatari ya kupatwa na mshituko wa moyo zaidi kuliko wanawake katika kipindi chote cha maisha hasa kabla ya wanawake hawajafikia wakati wa kukatika hedhi. Lakini kwa ujumla kwa kuwa wanawake huishi miaka mingi kuliko wanaume, magonjwa mengine ya moyo husababisha vifo vya wanawake uzeeni zaidi kuliko wanaume.
0 comments:
Post a Comment