TUMEELEZA kuhusu kansa ya tezi dume, leo tutafafanua vihatarishi vinavyochangia mwanamume kupata saratani ya tezi dume. Vifuatavyo ni baadhi yake: Kwanza kabisa ni umri. Nafasi ya kupata saratani ya tezi dume huongezeka sana hasa ukifikia umri wa karibu miaka 50 na kuendelea.
Nasaba ni kihatarishi kingine ambapo wanaume wenye historia ya tatizo hili kwenye familia zao, yaani wale ambao mmoja wa ndugu zao wamewahi kuugua ugonjwa huu huwa katika hatari ya kupata kansa hiyo kutokana na kurithi ‘gene’ za ugonjwa huo.
Suala lingine ni lishe ambapo wanaume wanaopenda kula nyama nyekundu (red meat) na walaji wa chakula chenye kiasi kikubwa cha mafuta hasa ya wanyama huwa katika hatari kubwa ya kupata saratani ya tezi dume.
Vilevile wanaume wasiopenda kufanya mazoezi, wanene na wenye upungufu wa virutubisho vya Vitamin E pia wako kwenye hatari zaidi ya kupata saratani ya kibofu cha mkojo. Wanaume wengine walio katika hatari kubwa ya kupata saratani ya tezi dume ni pamoja na wale wakulima wanaotumia aina fulani ya mbolea za kemikali, wanaofanya kazi katika viwanda vya kutengeneza matairi na wachimbaji madini, hususan aina ya cadmium.
Dalili za saratani ya tezi dume hazitofautiani na zile za kuvimba kwa tezi dume au BPH. Dalili hizo ni pamoja na, kupata shida wakati wa kuanza kukojoa, kutiririka kwa mkojo baada ya kumaliza kukojoa, kukojoa mkojo wenye mtiririko dhaifu, kukojoa mara kwa mara hasa nyakati za usiku, kujikakamua wakati wa kukojoa na kushindwa kumaliza mkojo wote na kutoa mkojo uliochanganyika na damu.
Pamoja na kueleza dalili hizo wapenzi wasomaji mnapaswa kutambua kuwa, mwanaume anapoanza kuona na kuhisi baadhi ya dalili hizo, anapaswa kujua kuwa, seli za saratani katika tezi dume lake huwa zina umri wa takribani miaka saba na kuendelea.
Iwapo saratani imesambaa mwilini kiasi cha kuhusisha sehemu nyigine za mwili, mgonjwa anaweza kuwa na maumivu makali ya mifupa katika maeneo ya nyonga, mapajani na kiunoni. Aidha mgonjwa huwa na dalili nyingine zinazoweza kumpata mgonjwa mwingine yeyote wa saratani kama vile kupungua uzito, kuhisi kichefuchefu, uchovu, kizunguzungu na kadhalika.
UCHUNGUZI
Kuna vipimo viwili ambavyo daktari anaweza kumpima mwanaume ikiwa ni hatua ya kwanza ya kugundua ugonjwa huo. Vipimo hivyo vya kwanza ni “Digital Rectal Exam (DRE)” na cha pili ni “Prostate Specific Antigen (PSA)”. DRE pamoja na PSA huonesha uwepo wa tatizo kwenye tezi dume, lakini vipimo hivi havina uwezo wa kutofautisha iwapo tatizo hilo linamaanisha saratani au uvimbe katika tezi dume. Hivyo basi, ili kuweza kutofautisha kati ya magonjwa hayo mawili, kipimo kiitwacho Prostate biopsy hufanywa.
Itaendelea wiki ijayo.
0 comments:
Post a Comment