Wasiliana Nasi

Wasiliana Nasi

Friday, December 5, 2014

FAHAMU UGONJWA WA SARATANI YA TEZI DUME (PROSTATE CANCER)-2


Wiki iliyopita nilianza kuelezea ugonjwa wa saratani ya tezi dume, leo nitafafanua dalili za ugonjwa huu kama ifuatavyo:

Daktari mmoja ambaye ni miongoni mwa waathirika wa saratani hiyo na mwanzilishi wa kampeni ya kuangamiza saratani ya tezi dume nchini Tanzania ya ‘50 Plus Campaign’ anasema kuwa, ugonjwa huu ukitambuliwa mapema huweza kutibika kwa urahisi.

Kuna vihatarishi vingi vinavyochangia mwanamume kupata saratani ya tezi dume. Vifuatavyo ni baadhi yake; kwanza kabisa ni umri. Nafasi ya kupata saratani ya tezi dume huongezeka sana hasa ukifikia umri wa karibu miaka 50 na kuendelea.

Nasaba ni kihatarishi kingine ambapo wanaume wenye historia ya tatizo hili kwenye familia zao, yaani wale ambao mmoja wa ndugu zao wamewahi kuugua ugonjwa huu huwa katika hatari ya kupata kansa hiyo kutokana na kurithi ‘gene’ za ugonjwa huo. Suala lingine ni lishe ambapo wanaume wanaopenda kula nyama au (red meat) na walaji wa chakula chenye kiasi kikubwa cha mafuta hasa ya wanyama huwa katika hatari kubwa ya kupata saratani ya tezi dume.

Wanaume wasiopenda kufanya mazoezi, wanene na wenye upungufu wa virutubisho vya Vitamin E pia wako kwenye hatari zaidi ya kupata saratani ya kibofu cha mkojo. Wanaume wengine walio katika hatari kubwa ya kupata saratani ya tezi dume ni pamoja na wale wenye asili ya Afrika (weusi) ikilinganishwa na wazungu, wakulima wanaotumia aina fulani ya mbolea za kemikali, wanaofanya kazi katika viwanda vya kutengeneza matairi na wachimbaji madini, hususan aina ya cadmium.

DALILI
Katika hatua zake za awali, dalili za saratani ya tezi dume hazitofautiani na zile za kuvimba kwa tezi dume au BPH. Dalili hizo ni pamoja na, kupata shida wakati wa kuanza kukojoa, kutiririka kwa mkojo baada ya kumaliza kukojoa, kukojoa mkojo wenye mtiririko dhaifu, kukojoa mara kwa mara hasa nyakati za usiku, kujikakamua wakati wa kukojoa na kushindwa kumaliza mkojo wote na kutoa mkojo uliochanganyika na damu.

Pamoja na kueleza dalili hizo wasomaji wanapaswa kutambua kuwa, mwanaume anapoanza kuona na kuhisi baadhi ya dalili hizo, anapaswa kujua kuwa, seli za saratani katika tezi dume lake huwa zina umri wa takribani miaka saba na kuendelea.

Iwapo saratani imesambaa mwilini kiasi cha kuhusisha sehemu nyingine za mwili, mgonjwa anaweza kuwa na maumivu makali ya mifupa katika maeneo ya nyonga, mapajani na kiunoni. Aidha mgonjwa huwa na dalili nyingine zinazoweza kumpata mgonjwa mwingine yeyote wa saratani kama vile kupungua uzito, kuhisi kichefuchefu, uchovu, kizunguzungu na kadhalika.

0 comments:

Post a Comment