Wasiliana Nasi

Wasiliana Nasi

Wednesday, September 3, 2014

UNAZIFAHAMU DALILI ZA SHAMBULIZI LA MOYO (HEART ATTACK)?

Moja ya magonjwa hatari sana ambayo yanaweza kumpata mtu yoyote ni ugonjwa wa shambulizi la moyo. Huu ni miongoni mwa magonjwa yanayoongoza kwa kusababisha vifo vya wanaume na wanawake.

Kwa kawaida, ugonjwa huu hutokea pale ambapo sehemu ya nyama ya moyo inapoharibika au kufa kutokana na kukosa damu ya kutosha.



Je tatizo hili husababishwa na nini?
Husababishwa na kuziba kwa mishipa ya damu inayosambaza damu katika moyo (coronary artery blockage) kutokana na mafuta mabaya mwilini (atherosclerotic plaque).

Watu gani wapo katika hatari ya tatizo hili?
Watu walio katika hatari ya kukumbwa na ugonjwa huu ni pamoja na
• Wavutaji wa sigara
• Wenye umri mkubwa miaka 45 kwa wanaume na 55 kwa wanawake
• Watu wenye mafuta ya lijamu katika damu au wale wenye mafuta mabaya aina ya triglycerides na low density lipoprotein kwa kiwango kikubwa katika damu zao
• Wenye kisukari
• Wenye matatizo ya shinikizo la damu
• Walio na unene kupita kiasi (obesity)
• Wenye matatizo sugu ya kushindwa kufanya kazi kwa figo zao (chronic renal failure)
• Moyo kushindwa kufanya kazi (heart failure)
• Wanywaji wa pombe kupindukia
• Watumiaji wa madawa ya kulevya hasa cocaine na methamphetamine
• Watu wenye msongo wa mawazo (Chronic high stress levels)
• Upungufu wa vitamin B2, B6, B12 na folic acid

Dalili za shambulizi la moyo
• Maumivu makali ya ghafla kifuani ambayo husambaa kwenye taya, shingo, bega na mkono wa kushoto
• Kupumua kwa shida
• Kutoka jasho kwa wingi sana (diaphoresis)
• Kuhisi mapigo ya moyo yanapiga haraka (palpitations)
• Kichefuchefu
• Kutapika
• Kuchoka haraka sana
• Kupoteza fahamu
Shambulizi la moyo limehusishwa na nini?
Tafiti mbalimbali zimeusisha mambo yafuatayo na shambulizi la moyo
• Msongo wa mawazo
• Maambukizi hasa vichomi vinavyosababishwa na vimelea vya chlamydophila pneumonia.
• Hutokea zaidi asubuhi hasa saa tatu (saa 3 asubuhi)

Vipimo na uchunguzi
• ECG - Kipimo hiki huonyesha ni sehemu gani ya moyo iliyoathirika
• Coronary angiography - Kinasaidia kwa kuangalia wapi ambapo mishipa ya damu imekuwa membamba sana kupita kiasi (narrowing of vessels) au imeziba.
• Cardiac markers levels
• X-ray ya kifua (chest X-ray)
• MPI (Myocardial Perfusion Imaging) - Kipimo hiki hufanywa kwa kutumia mashine maalum ya PET Scan ambapo kinauwezo wa kugundua tatizo la shambulizi la moyo, huchunguza kikamilifu maumivu ya kifua, huangalia mwelekeo wa tiba ya kuzuia damu kuganda, hutoa mwelekeo wa ugonjwa wa shambulizi la moyo kama ni mzuri au mbaya, hutathmini ubora wa tiba ya shambulizi la moyo kabla na baada ya mgonjwa kupata tiba, huweza kutambua hata shambulizi la moyo ambalo si rahisi kugundulika kwa kutumia vipimo vyengine na pia hutathmini ukubwa wa tatizo la shambulizi la moyo. Hata hivyo kwa sasa kipimo hiki hakipatikani nchini kwetu.

Ili kuweza kutambua uwepo wa tatizo hili, mwaka 1979, shirika la Afya Duniani (WHO) liliweka vigezo vya kutambua shambulizi la moyo. Vigezo hivyo ni
• Historia ya kuwa na maumivu ya kifua zaidi ya dakika 20
• Mabadiliko katika kipimo cha ECG, na
• Kupanda na kushuka kwa kipimo kiitwacho kitaalamu cardiac biomarkers hasa creatine kinase - MB na troponin

Matibabu

Shambulio la moyo ni tatizo linalohitaji matibabu ya dharua. Lisipotibiwa kwa haraka husababisha kifo katika muda mfupi sana tangu mgonjwa apatwe na tatizo. Matibabu ya tatizo hili hujumuisha
• Kumpa mgonjwa hewa ya oksijeni
• Mgonjwa hupewa vidonge vya Aspirini ndogo kuzuia damu kuganda (thrombolytic) kwa ajili ya kuyeyusha damu iliyaganda na hivyo kuzibua mirija midogo ya damu katika moyo iliyozibwa na kuganda huku kwa damu.
• Vile vile mgonjwa hupewa dawa za kuweka chini ya ulimi kiitwacho nitrogylycerin (glyceryl trinitrate) ambazo husaidia kutanua mishipa ya damu (vasodilation)
• Dawa ya kutuliza maumivu kwa mfano morphine
• Dawa ya kuyeyusha mafuta katika mishipa ya damu kama vile clopidogrel
• Kuzibua mishipa ya damu inayosambaza damu katika moyo kwa kutumia - Percutaneous coronary intervention (PCI)
• Upasuaji (CABG)

Njia za kuzuia shambulizi la moyo
• Kuacha kuvuta sigara
• Kufanya mazoezi ya mara kwa mara
• Kupunguza unywaji wa pombe
• Kubadilisha aina ya mlo. Kupunguza mafuta katika mlo na chumvi.
• Kutumia mafuta ya samaki (omega-3 fatty acids)
• Kuna utafiti unaosema kuwa uchangiaji damu hupunguza hatari ya magonjwa ya moyo hasa kwa wanaume.

Madhara ya shambulizi la moyo
• Moyo kushindwa kufanya kazi (heart failure)
• Matatizo katika mfumo wa mapigo ya moyo (Atrial fibrillation) ambayo hatimaye hupelekea kifo
• Shambulizi la moyo kurudia mara ya pili
• Kifo cha ghafla (sudden death)

0 comments:

Post a Comment