Na Haruni Sanchawa/Uwazi
MAITI ya Mchungaji James Regnald Mhando aliyefariki Februari 18,
mwaka huu imezua tafrani nzito kwa ndugu na jamaa baada ya kujulikana
kuwa alikuwa na wake wawili ambapo mke mmoja alitaka mwili uagwe
hospitali na upande wa pili ukitaka ukaagwe kwa mama yake marehemu.
Mchungaji James Regnald Mhando enzi za uhai wake. Katika
msiba huo ilibainika kuwa, mchungaji huyo (kanisa lake tunalihifadhi
kwa sababu maalum), alikuwa na watoto sita kwa mama tofauti na wote
walijitokeza katika mazishi ya baba yao.
Inadaiwa kuwa
Mchungaji Mhando alianza kuumwa Jumamosi ya Februari 14, mwaka huu
lakini inadaiwa baadhi ya watoto na ndugu wengine hawakujulishwa hadi
Jumanne ambapo inadaiwa alibebwa na gari la wagonjwa kutokea Morogoro
hadi Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Jeneza la mchungaji James Regnald Mhando. Habari
zinasema ilipofika Jumatano saa tano usiku, mchungaji huyo aliaga dunia
na mbali ya kuaga dunia, bado tukio hilo lilikuwa ni siri na ilidaiwa
ilikuwa afanyiwe shughuli za mazishi kwa siri bila ya baadhi ya watoto
wake wakubwa kujua.
Hata hivyo, habari za msiba huo zilizagaa
haraka na kumfikia mke wa kwanza wa ndoa ambaye alikuwa nchini kwa ajili
ya mapumziko kwani anafanya kazi nje ya nchi, hivyo ukoo ukaanza
kutaarifiana.
Mchungaji Mhando alioa na kufunga ndoa Novemba 17,
1979 katika Kanisa la Anglikana la Mtakatifu Albano, jijini Dar es
Salaam, hata hivyo, ilidaiwa kuwa mwaka 1985 mtumishi huyo wa Mungu
aliamua kuondoka nyumbani alikokuwa akiishi na mkewe na kwenda kuishi na
mwanamke mwingine ambaye inadaiwa kuwa alikuwa ni wa dhehebu lingine na
wakafunga ndoa serikalini.
Habari zinadai kwamba mwanamke huyo
alikuwa anaitwa Mwanaheri kabla ya kubadili dini na kuitwa Glory na
wakafanikiwa kuzaa watoto wawili, mmoja akapewa jina la Reginald Junior
na mtoto mwingine anaitwa Sada au Doreen Mhando. Habari zinasema kabla
ya kuondoka kwa mke wa kwanza, mchungaji huyo alizaa naye watoto wawili,
wa kiume na wa kike.
...Askari akiwa eneo la tukio. Hata
hivyo, wakati wa msiba huo watoto wengine wawili walijitokeza nao
wakidai kuwa ni baba yao, hali iliyozusha minong’ono kwa watu
walioshangazwa na mwenendo wa marehemu.Akizungumza na Uwazi, mama mzazi
wa mchungaji huyo aliyejitambulisha kwa jina la Dorofea Mhando (82)
alisema kitendo kilichofanywa na mwanamke huyo ni kibaya kwani
alimshawishi mwanaye kuisaliti familia yake.
“Mwanamke huyo
mwingine alikuwa akiishi na mwanangu kwa siri kubwa sana, kama vile
marehemu hakuwa na familia na akawa anajifanya kuwa yeye ndiye mke wa
kwanza, kitu ambacho ni cha uongo kwani marehemu alishaoa kanisani mwaka
1979.
“Marehemu baada ya kumpata mwanamke huyo alikuwa
hashiriki shughuli nyingi za hapa nyumbani kwa kuhofia watu watajua
kuwa alikuwa na familia nyingine, kitu ambacho kilinisikitisha,” alidai
mama huyo.
Mwili wa marehemu ukiagwa. Mama
huyo aliongeza kuwa maisha ya mchungaji huyo yalikuwa sehemu mbili,
Morogoro na jijini Dar es Salaam, alikuwa akifikia Mivinjeni kwenye
ofisi ya shughuli zake.“Baada ya kupata taarifa ya msiba niliagiza mwili
uletwe hapa Ukonga Majumba Sita ukitokea Muhimbili kwa ajili ya
shughuli za kuagwa lakini mke mdogo akawa anapinga,” alidai mama huyo.
Hata
hivyo, ilidaiwa kuwa mke mdogo alisisitiza kuwa baada ya kuandaa mwili
wa marehemu uagwe Muhimbili, kisha upelekwe katika Makabauri ya
Kinondoni kwa mazishi. Kulitokea mabishano ambapo mtoto mkubwa wa
marehemu aliyefahamika kwa jina Feda, alisema baba yao hawezi kuagwa
kama mkimbizi kwani ana watoto, mke na mama yake mzazi, hivyo akaamuru
mwili ukaagwe kwa bibi yake Ukonga Majumba Sita.
Habari zinadai
kuwa mvutano huo ulifikishwa Polisi Kituo Kikuu ambapo lilifunguliwa
jalada namba CD/ RB/ 2627/ 2015 ambao waliamuru shughuli za mazishi
zisifanyike hadi muafaka upatikane.
Habari zinadai kikao kilifanyika polisi na muafaka ukapatikana kwamba mwili ukaagwe kwa mama yake mzazi Ukonga Majumba Sita.

Maofisa
wa polisi walitoa askari wenye silaha chini ya kamanda wao
aliyefahamika kwa jina moja la Manyama aliyeongozana na wana familia hao
hadi Muhimbili kisha Ukonga, baadaye kwenye Makaburi ya Kinondoni
ambapo mchungaji huyo alizikwa chini ya ulinzi.