Wasiliana Nasi

Wasiliana Nasi

Sunday, July 6, 2014

THE FADHAGET SANITARIUM CLINIC LEO INAKUPA SOMO LA KUKABILIANA NA KANZA YA MATITI


CONCHITA hakuwa na dalili zozote za kansa.Alikuwa na umri wa miaka 40, mwenye afya nzuri, na hakuna mtu yeyote katika familia yao aliyewahi kuugua ugonjwa huo. Eksirei ya matiti ambayo alipigwa kwa ukawaida haikuonyesha tatizo lolote. Lakini siku moja alipokuwa akijichunguza mwenyewe akiwa bafuni, alihisi uvimbe fulani. Uvimbe huo uligunduliwa kuwa kansa. Conchita na mume wake waliketi wakiwa wamechanganyikiwa huku daktari akiwaeleza kuhusu matibabu mbalimbali wanayoweza kuchagua.

Zamani, daktari angemwambia mwanamke aliye na kansa ya matiti kwamba matibabu pekee ni kukatwa titi kabisa, upasuaji ambao uliacha kovu kubwa sana kwa kuwa ulihusisha kukata titi, tezi za limfu kwenye kifua na kwapa, na misuli ya kifua. Mara nyingi kutibiwa kwa kutumia kemikali au miale kulifanya hali iwe mbaya hata zaidi. Kwa sababu hiyo, watu wengi waliogopa matibabu ya ugonjwa huo kuliko ugonjwa wenyewe.

Jitihada nyingi zimefanywa ili kutibu kansa hiyo hatari ya matiti bila kumwacha mgonjwa na kovu kubwa na athari za matibabu. Kama ilivyokuwa katika kisa cha Conchita, leo wagonjwa walio na kansa ya matiti wanaweza kuchagua matibabu mbalimbali.* Na utafiti wa kitiba unaoendelea kufanywa pamoja na ripoti za kitiba kwenye vyombo vya habari zinawapa watu tumaini kwamba matibabu mapya, mbinu mpya za kuchunguza ikiwa mtu yuko katika hatari ya kupatwa na ugonjwa huo, na kula vyakula vinavyoimarisha mfumo wa kinga hatimaye zitamaliza ugonjwa huo.


Hata hivyo, licha ya maendeleo ya kitiba, bado kansa ya matiti ndiyo kansa inayosababisha vifo vingi zaidi vya wanawake.* Nchi zilizoendelea za Amerika Kaskazini na Ulaya Magharibi ndizo zenye idadi kubwa zaidi ya watu walio na kansa, lakini idadi ya wanawake walio na kansa ya matiti inaongezeka katika bara la Asia na Afrika ambako kwa kawaida kumekuwa na idadi ndogo. Kwa kweli, idadi ya wanaokufa kati ya wale wanaogunduliwa kuwa na ugonjwa huo huko Asia na Afrika ni ya juu. Kwa nini? Daktari mmoja barani Afrika anasema: “Kansa hiyo haigunduliwi mapema. Wagonjwa wengi huja ikiwa tayari imeenea sana.”

Hatari ya kupatwa na kansa hiyo huongezeka kadiri umri unavyosonga. Asilimia 80 hivi ya wanawake wenye kansa ya matiti wana umri unaozidi miaka 50. Lakini jambo linalofariji ni kwamba kansa ya matiti ni mojawapo ya kansa zinazoweza kutibiwa kwa urahisi. Kwa kweli, asilimia 97 ya wanawake nchini Marekani waliotibiwa kabla ya kansa hiyo kuenea wangali hai miaka mitano baada ya kansa hiyo kugunduliwa. Kufikia sasa, miaka mitano imepita tangu kansa ya Conchita ilipogunduliwa.

Mambo ya Msingi Kuhusu Kansa ya Matiti

Kama katika kisa cha Conchita, mara nyingi kansa ya matiti huanza kama uvimbe usio wa kawaida. Jambo lenye kufariji ni kwamba asilimia 80 hivi ya uvimbe huo si hatari bali ni vifuko vyenye umajimaji.

Kansa ya matiti huanza wakati ambapo chembe moja inajigawanya haraka sana isivyo kawaida na bila utaratibu, na hatua kwa hatua inafanyiza uvimbe. Uvimbe unakuwa kansa wakati chembe zake zinapovamia tishu nyingine. Uvimbe fulani unaweza kukua kwa haraka; mwingine unaweza kuchukua miaka kumi hivi kabla ya kugunduliwa.

Ili kuchunguza ikiwa uvimbe wa Conchita ulikuwa na kansa, daktari wake alitumia sindano nyembamba kutoa tishu kutoka kwenye uvimbe huo. Uvimbe huo ulikuwa na kansa. Hivyo, alifanyiwa upasuaji ili kuondoa uvimbe huo na tishu zilizozunguka titi. Upasuaji huo ulisaidia pia kuonyesha uvimbe huo ulikuwa umefikia hatua gani (ukubwa, aina, na kuenea kwake) na kuchunguza ulikuwa ukikua upesi kwa kadiri gani.

Baada ya upasuaji, wagonjwa wengi hupata matibabu mengine ambayo yatazuia kansa isirudi au kuenea. Chembe zenye kansa zinaweza kutoka kwenye uvimbe na kusafiri kupitia mfumo wa damu au mfumo wa limfu, na kuanza kukua tena mahali pengine mwilini. Kuenea kwa kansa hadi kwenye viungo na tishu muhimu kama vile ubongo, ini, uboho wa mfupa, au mapafu ndio hufanya ugonjwa huo uwe hatari.

Conchita alitibiwa kwa miale na kemikali ili kuharibu chembe za kansa kwenye titi na pia katika sehemu nyingine za mwili. Kwa kuwa uvimbe wenye kansa aliokuwa nao ulichochewa hasa na homoni ya estrojeni, alipewa matibabu ya kuzuia kutokezwa kwa homoni hiyo ili kuzuia uvimbe mpya wenye kansa usitokee.

Kwa sababu ya maendeleo katika matibabu ya kansa ya matiti, kumekuwa na matibabu mbalimbali ikitegemea umri, afya, historia ya kansa katika familia, na aina ya kansa. Kwa mfano, katika kisa cha mwanamke anayeitwa Arlette, uchunguzi ulifanya kansa yake igunduliwe kabla haijaenea nje ya vijia vya kupitishia maziwa. Kwa hiyo, alifanyiwa upasuaji wa kuondoa uvimbe huo, na titi lake halikukatwa. Kabla ya kufanyiwa upasuaji, Alice alitibiwa kwa kemikali ili kupunguza ukubwa wa uvimbe. Daktari wa Janice aliondoa tu uvimbe na tezi za limfu zilizokuwa karibu, ambazo huwa za kwanza kuingia umajimaji kutoka kwenye uvimbe. Kwa kuwa tezi nyingine hazikuwa na chembe zenye kansa, hakuziondoa. Hilo lilifanya mkono wa Janice usivimbe kwa sababu ya kufungika kwa mishipa ya limfu, jambo ambalo hutokea wakati tezi nyingi za limfu zinapoondolewa.

Utafiti mwingi umefanywa kuhusu ukuzi wa kansa ya matiti, lakini swali la msingi ni, Ni nini husababisha kansa ya matiti, nayo huanza jinsi gani?

Visababishi Ni Nini?

Visababishi vya kansa ya matiti bado ni fumbo. Wachambuzi wanasema kwamba utafiti mwingi unafanywa kuhusu tiba na kuchunguza ikiwa mtu ana kansa hiyo—jambo ambalo linaleta faida kubwa—badala ya kutafuta visababishi vyake na jinsi ya kuizuia. Hata hivyo, wanasayansi wamegundua mambo kadhaa muhimu. Wengine wanaamini kwamba kansa ya matiti hutokana na hatua nyingi tata ambazo huanza wakati ambapo chembe fulani ya urithi yenye kasoro inapofanya chembe zitende kwa njia isiyo ya kawaida, yaani, zigawanyike kwa kasi sana, zishambulie tishu nyingine, na kuepuka kuharibiwa na mfumo wa kinga, kisha pole kwa pole chembe hizo zinashambulia na kuharibu viungo muhimu vya mwili.

Chembe hizo za urithi zenye kasoro hutoka wapi? Asilimia 5 hadi 10 ya visa vya kansa hiyo huonyesha kwamba wanawake huzaliwa na chembe za urithi ambazo zinaweza kusababisha kansa ya matiti. Lakini inaonekana kwamba katika visa vingi, chembe za urithi zenye afya huharibiwa na vitu vingine vilivyo nje ya mwili kama vile, miale na kemikali. Huenda utafiti wa wakati ujao ukathibitisha jambo hilo.

Jambo lingine linalohusianishwa na kansa ya matiti ni homoni ya estrojeni ambayo huenda inachochea aina fulani za kansa hiyo. Kwa hiyo, mwanamke anaweza kupatwa na kansa hiyo ikiwa alianza kupata hedhi mapema maishani au ikiwa aliacha kupata hedhi akiwa amechelewa isivyo kawaida, ikiwa alipata mimba ya kwanza umri wake ukiwa umesonga au ikiwa hakuwahi kupata mimba, au ikiwa alipata matibabu ya kurudisha homoni fulani mwilini. Kwa kuwa chembe za mafuta hutokeza estrojeni, huenda wanawake walionenepa kupita kiasi waliofika umri wa kuacha kupata hedhi na hivyo ovari zao hazitokezi tena homoni, wakawa katika hatari ya kupatwa na kansa hiyo. Pia watu walio na viwango vya juu vya insulini na watu walio na viwango vya chini vya homoni ya usingizi inayoitwa melatonin, kama vile watu wanaofanya kazi usiku, wako pia katika hatari ya kupatwa na kansa hiyo.

Je, kuna tumaini lolote la kugunduliwa kwa tiba bora ya kansa ya matiti isiyotokeza madhara? Watafiti wanachunguza matibabu ambayo yatahusisha kutumia mfumo wa kinga wa mwili na dawa ambazo zitalenga hasa utendaji wa chembe za urithi na protini ambazo huchochea ukuzi wa kansa. Kwa sasa, teknolojia iliyoboreshwa ya kupiga picha za eksirei inapaswa kuwasaidia madaktari kutibu kwa njia hususa kwa kutumia miale.

Wanasayansi pia wanajifunza mambo mengine kuhusu kansa kutia ndani: kuelewa ni kwa nini kansa huenea, kudhibiti chembe za kansa ambazo haziharibiwi kupitia matibabu ya kemikali, kuzuia kugawanyika kwa chembe, na kutibu kila uvimbe kwa njia hususa.

Hata hivyo, katika ulimwengu wa leo, magonjwa hayawezi kuondolewa kabisa na wanadamu wataendelea kufa. (Waroma 5:12) Ni Muumba wetu tu anayeweza kubadili hali hiyo yenye kusikitisha. Je, atafanya hivyo? Biblia inajibu, ndiyo! Inasema kwamba kutakuwa na wakati ambapo “hakuna mkaaji atakayesema: ‘Mimi ni mgonjwa.’”* (Isaya 33:24) Hicho kitakuwa kitulizo kwelikweli!

Baadhi ya majina yamebadilishwa. Amkeni! halipendekezi matibabu yoyote hususa. Idadi ya wanaume wanaopatwa na kansa ya matiti ni ndogo sana ikilinganishwa na ya wanawake.

Ahadi hiyo inazungumziwa kwa urefu katika kitabu Biblia Inafundisha Nini Hasa? kilichochapishwa na Mashahidi wa Yehova.

DALILI UNAZOPASWA KUANGALIA

Ugunduzi wa mapema ni muhimu, lakini utafiti fulani unaonya kwamba huenda uchunguzi wa matiti na eksirei ya matiti kwa wanawake wachanga isitoe habari sahihi na hivyo kufanya wapate matibabu wasiyohitaji na kuwa na wasiwasi. Hata hivyo, wataalamu wanawahimiza wanawake waangalie mabadiliko yoyote katika matiti yao na mfumo wao wa limfu. Zifuatazo ni baadhi ya dalili unazopaswa kuangalia:

● Uvimbe wowote au kuongezeka kwa unene wa ngozi kwenye makwapa au titi

● Umajimaji wowote unaotoka kwenye chuchu ambao si maziwa

● Mabadiliko yoyote ya rangi au ngozi ya titi

● Chuchu iliyodidimia kwa njia isiyo ya kawaida au inayowasha

UNAPOGUNDULIWA UNA KANSA YA MATITI

● Tazamia kwamba itakuchukua zaidi ya mwaka mmoja kutibiwa na kupata nafuu.

● Ikiwezekana, chagua madaktari wenye ujuzi ambao wataheshimu mahitaji na imani yako.

● Mkiwa familia, amueni ni nani mtakayemwambia kuhusu ugonjwa wako, na mtafanya hivyo wakati gani. Hilo litawawezesha marafiki wenu waonyeshe upendo na kusali nanyi na kwa niaba yenu.—1 Yohana 3:18.

● Kabiliana na mkazo wa kihisia kwa kusoma Biblia, kusali, na kutafakari mambo yanayofaa.—Waroma 15:4; Wafilipi 4:6, 7.

● Zungumza na wale ambao wamewahi kuugua kansa ya matiti na watakaokutia moyo.—2 Wakorintho 1:7.

● Jaribu kukazia fikira mahangaiko ya leo tu, na si ya kesho. Yesu alisema: “Msihangaike kamwe juu ya kesho, kwa maana kesho itakuwa na mahangaiko yake yenyewe.”—Mathayo 6:34.

● Tumia vizuri nguvu zako. Unahitaji kupumzika vya kutosha.

KUZUNGUMZA NA DAKTARI WAKO

● Jifunze maneno machache ya kitiba kuhusu kansa ya matiti.

● Kabla ya kwenda kumwona daktari, andika orodha ya maswali, na umwombe mwenzi wako au rafiki aandamane nawe ili akusaidie kuandika mambo machache.

● Daktari wako akisema jambo ambalo huelewi, mwombe akufafanulie zaidi.

● Mwulize daktari wako ametibu watu wangapi wenye kansa kama yako.

● Ikiwezekana, tafuta maoni ya daktari mwingine.

● Ikiwa madaktari wako wanatofautiana, chunguza ujuzi wa kila mmoja wao wa kutibu kansa hiyo. Waombe wajadiliane kuhusu hali yako. Unaweza pia kutafuta maoni ya daktari mwingine.

KUKABILIANA NA ATHARI ZA MATIBABU

Huenda matibabu fulani yakatokeza athari kama vile kichefuchefu, nywele kung’oka, kujihisi mchovu sana, maumivu, kufa ganzi au kuwashwa kwenye mikono na miguu, na matatizo ya ngozi. Hatua zifuatazo zinaweza kupunguza athari hizo:

● Kula chakula kizuri ili mfumo wako wa kinga uwe na nguvu.

● Weka rekodi inayoonyesha jinsi nishati yako inavyobadilika na jinsi unavyoathiriwa na vyakula mbalimbali.

● Jaribu kupunguza kichefuchefu na maumivu kwa kutumia dawa, tiba ya kuchoma kwa sindano ili kuamsha mishipa ya fahamu, au kukandwa mwili.

● Fanya mazoezi ya kiasi ili uwe na nguvu, udhibiti uzito wako, na kuboresha utendaji wa mfumo wako wa kinga.*

● Pumzika mara nyingi, lakini zingatia kwamba kulala kwa muda mrefu huongeza uchovu.

● Usiache ngozi yako ikauke. Vaa nguo ambazo hazikubani. Oga kwa maji yenye joto.

Watu wanaougua kansa wanapaswa kumwona mtaalamu wa kitiba kabla ya kuanza kufanya mazoezi yoyote.

IKIWA MTU UNAYEMPENDA ANA KANSA

Unaweza kumtegemeza jinsi gani mpendwa aliye na kansa? Fuata kanuni hii ya Biblia: “Shangilieni pamoja na watu wanaoshangilia; lieni pamoja na watu wanaolia.” (Waroma 12:15) Mwonyeshe kwamba unampenda na kumjali kupitia simu, barua, kadi, barua pepe, na kumtembelea kwa muda mfupi. Salini pamoja, na kusoma maandiko yenye kufariji kutoka kwenye Biblia. Beryl, ambaye mume wake ni mwangalizi anayesafiri wa Mashahidi wa Yehova, anahimiza hivi: “Usiwataje watu waliokufa kutokana na kansa, lakini taja wale ambao bado wako hai.” Janice, ambaye wakati mmoja aliugua kansa anasema hivi: “Nenda tu na umkumbatie rafiki yako. Akitaka kuzungumza kuhusu hali yake, atafanya hivyo.” Waume hasa wanahitaji kuwahakikishia wake zao kwamba wanawapenda.

“Mara kwa mara, tulikuwa na siku ambayo hatukuzungumza kuhusu kansa,” anasema Geoff. “Mke wangu alikuwa ameazimia kwamba hatutakazia fikira afya yake tu. Kwa hiyo tuliamua kwamba mara kwa mara, kwa siku nzima, hatutazungumza kuhusu kansa. Badala yake, tulikazia fikira mambo mengine mazuri katika maisha yetu. Ni kana kwamba tulichukua likizo kutokana na ugonjwa huo.”

0 comments:

Post a Comment